Imeelezwa kuwa, matumizi ya nishati
safi ya kupikia ni ajenda ya kitaifa
inayolenga kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi na salama ya kupikia
ikiwemo nishati ya umeme.
Aidha, takwimu za mwaka 2022
zinaonesha kuwa Watanzania wanaotumia nishati ya umeme kwa ajili ya kupikia ni
asilimia 4.2 tu huku ikitajwa kuwa idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na idadi
ya watanzania waliopo.
Akizungumza Agosti 14, 2025 jijini
Dodoma wakati akizindua Mpango wa Ugawaji Majiko ya Kupikia kwa Umeme kwa
Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Naibu Waziri Mkuu na Waziri
wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa kutokana na historia ya siku za
nyuma Watanzania walidhani kuwa kupika kwa umeme ni ghali zaidi tatizo ambalo lilisababishwa
na masuala mengi ikiwemo elimu kuhusu unafuu wa gharama kwa matumizi ya umeme.
“Utafiti wa TANESCO unaonesha kuwa
kupikia kwa nishati ya umeme, hasa kwa kutumia majiko janja yenye ufanisi ni nafuu zaidi kuliko wanavyofikiria wengi
miongoni mwetu katika jamii tunazoishi. Utafiti huo unaonesha kuwa, majiko
janja ya umeme yanaweza kutumia chini ya uniti moja (1) ya umeme ambayo ni sawa
na chini ya shilingi za Kitanzania 352 kuandaa mlo mmoja,” amesema Dkt. Biteko.
Amefafanua kuwa matumizi ya umeme kwa
ajili ya kupikia ni nafuu kuliko nishati nyingine hivyo Watanzania hawana haja
ya kuogopa kutumia umeme. Aidha, hatua ya Ugawaji Majiko ya Kupikia kwa Umeme
kwa Wafanyakazi TANESCO itakuwa hatua muhimu katika mabadiliko kwa kuwa
wafanyakazi hao wa TANESCO watakuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya
kupikia hususan majiko ya umeme katika
jamii.
“ Kupitia mpango huu, nimejulishwa
kuwa TANESCO, kwa kushirikianana Taasisi
ya Modern Energy Cooking Services (MECS) chini ya Serikali ya Uingereza imeweza
kununua zaidi ya majiko 11,000. Majiko haya yatawafikia wafanyakazi wote
waTANESCO kwa mpango wa mfuko wa mzunguko (revolving fund). Pia zimewekwa mbinu
bunifu za ugharamiaji ambazo ni rafiki kwa kila mtumiaji,”amesisitiza Dkt.
Biteko.
Amewapongeza wafanyakazi wa TANESCO
kuwa kufanya kazi kubwa ya kuwahudumia Watanzania kwa kuboresha utoaji wa
huduma ya umeme nchini na kuwaasa kuwa wabunifu zaidi katika kutekeleza
majukumu yao sambamba na kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya kwa jamii.
Kuhusu
programu hiyo ya Ugawaji wa Majiko ya Kupikia kwa Umeme amesema hapo baadaye itahusisha
wateja wa TANESCO wanaojiunga na huduma
ya umeme.
“ Wateja hao watapatiwa majiko na watalipa
kidogo kidogo kupitia manunuzi ya umeme (On bill financing) ilikuleta manufaa
zaidi kwa jamii nzima ya Tanzania. Nawaomba TANESCO kuharakisha jambo hili
iliwananchi waweze kunufaikana program hii muhimu,” ameeleza Dkt. Biteko.
Aidha, ametoa wito kwa Taasisi za Umma
na Binafsi kujifunza kutoka TANESCO na kaungalia namna ambavyo watumishi wao
wanaweza kunufaika na programu hiyo na kuchochoea matumizi ya nishati safi ya
kupikia hususani kwa kutumia umeme.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko
amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuwa kinara wa ajenda wa nishati safi ya kupikia na kuelekeza
wananchi wahamasishwe katika matumizi wa nishati safi ya kupikia.
Amebainisha kuwa hakuna mafanikio yoyote yaliyopatikana katika
nishati ya umeme na mafuta bila kumtaja Rais Samia ambaye ametoa msukumo mkubwa
katika seka hiyo si tu nchini Tanzania bali Afrika na duniani kote.
Aidha, amesema kuhusu hali ya umeme nchini,
takwimu zinaonesha kuwa, hadi kufikia Julai 2025, Tanzania ilikuwa na uwezo wa
kuzalisha jumla ya megawati 2,720. Ambapo mahitaji ya umeme kwenye Gridi ya
Taifa yamefikia megawati 1,921 pekee.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith
Kapinga kwa upande wake, amesema kuwa, tukio la ugawaji wa majiko ya umeme kwa
bei ya ruzuku kwa Wafanyakazi wa TANESCO
ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Nishagi Safi ya Kupikia ambayo
kinara wake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan.
Amesema zoezi hilo la ugawaji majiko
hayo ya umeme ni kielelezo cha kuwa, Wizara ya Nishati na Taasisi zake
zinaibeba Ajenda ya Nishati Safi ya
Kupikia kwa vitendo na pia inawafanya
wafanyakazi kuwa vinara na mabalozi wa
nishati safi ya kupikia.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Rosemary Senyamule amemshukuru Rais Samia kwa kuimarisha miradi ya nishati
katika Mkoa husika kwani katika kipindi cha miaka minne ametoa shilingi bilioni
214.3 ambazo zimekamilisha miradi ya umeme vijijini na kupekeka umeme kwenye
miradi mbalimbali ikiwemo umwagiliaji, afya na maji.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia,
amesema katika Mkoa wa Dodoma majiko ya gesi takriban 10,000 yamefikia
wananchi, pia miradi ya umeme jua na
upepo imefikia miradi mbalimbali ikiwemo ya umwagiliaji, na taasisi mbalimbali
zinatumia nishati safi ya kupikia ikiwemo vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama
pamoja na Shule mbalimbali.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,
Lazaro Twange alisema kuwa, tukio la ugawaji wa majiko ya umeme kwa TANESCO ni
muhimu kwani ni sehemu ya mpango mkakati
wa kuitikia wito wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha kuwa ifikapo
2034 asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia.
Amesema majiko yatakayosambazwa ni
11,000 na yatafikia watumishi wote wa
TANESCO, na hivyo ametoa wito kwa wafanyakazi kutumia majiko hayo na kuwa
mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya nisahati safi ya iupilia.
Mpango huo wa ugawaji majiko ya umeme
amesema.kuwa, unahusisha utoaji wa elimu,
usambazaji majiko na pia wananchi kukopeshwa majiko ya umeme ambapo
baadaye wataweza kulipa jinsi wanavyolipia umeme lengo likiwa ni kuongeza watu
wanaotumia umeme kupikia na hivyo shirika kuongeza mapato.
Mwakilishi wa mradi wa MECS uliopo
chini ya Serikali ya Uingereza, ambao
ndio umetoa majiko hayo ya umeme kwa
wafanyakazi wa TANESCO kwa bei ya ruzuku, Charles Barnabas amesema majiko hayo
yanatumia umeme kidogo.
Amesema pia wana kampeni ya kitaifa ya
Pika smart ambayo wanafanya na Tanesco ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi
ya kupikia kwa kutumia majiko ya umeme.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni