WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa vyama vya
wafanyakazi barani afrika kuweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya
teknolojia duniani.
Amesema kwa kufanya hivyo kutawawezesha kupunguza hatari ya
kupoteza ajira kutokana na ujio wa mashine pamoja na matumizi ya teknolojia
mpya ikiwemo za akili mnemba.
Ameyasema hayo leo (Ijumaa 22 Agosti 2025,) Alipomwakilisha
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi Afrika (OAUUT) uliofanyika Hoteli ya Johari Rotana Dar es Salaam.
Amesema kuwa, katika dunia ya sasa, imeshuhudiwa uwepo wa
mabadiliko makubwa yanayochagizwa na mapinduzi ya kiteknolojia ikiwemo matumizi
ya akili mnemba pamoja na utandawazi.
“Kuna hatari ya watu kupoteza ajira zao kadri mitambo na
mifumo ya kisasa inavyochukua kazi ambazo kwa kawaida zingeweza kufanywa na
wafanyakazi. Tunapaswa kuweka mpango wa kutoa mafunzo endelevu yanayoendana na
mabadiliko ya teknolojia ili kuwandaa wafanyakazi na aina mpya za ajira
zinazojitokeza.”
Amesema kuwa Tanzania kwa upande wake chini ya uongozi wa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko
hayo ikiwemo kuhamasisha matumizi sahihi ya teknolojia mpya ikiwemo akili
mnemba na kusisitiza ulinzi wa haki na faragha za wafanyakazi. “Teknolojia
lazima ilinde utu na si kudhoofisha heshima ya kazi.”
Amesema eneo lingine ni kuwajengea uwezo wafanyakazi kupitia
programu mbalimbali zitakazowawezesha kuwaongezea ujuzi katika kazi. “Tunafanya
hivi ili kuhakikisha watu wetu hasa vijana wanajengewa maarifa na stadi
zinazohitajika hasa katika maeneo ya
uchumi wa kijani na kidijitali.”
Aidha, amesema Serikali inathamini na kutambua mchango
mkubwa wa vyama vya wafanyakazi nchini na itaendelea kushirikiana nao katika
kuboresha masilahi ya wafanyakazi.
"Serikali imevipa nafasi vyama vya wafanyakazi kufanya
kazi kwa Uhuru na bila kuingiliwa tunawasihi kuendelea kushauriana na
kushirikiana na Serikali ili kuendelea kuboresha maslahi na mazingira ya
ufanyaji kazi."
Amesema ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali na vyama
hivyo umeiwezesha Serikali kutekeleza mahitaji yote muhimu ya wafanyakazi
nchini, ikiwemo maboresho ya Sera, Sheria na maslahi ya wafanyakazi.
Kadhalika, amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kuunga
mkono jitihada za Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Afrika (OAUUT) ikiwa ni
sehemu ya kuenzi jitihada za Baba wa Taifa ambae ni mwanzilishi wa Shirikisho
hilo.
Naye Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas
Katambi, amesema Serikali imeendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi
nchini na imepitisha Sera na Sheria mbalimbali katika kuhakikisha inarekebisha
na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Kwa Upande wake, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya
Wafanyakazi Afrika (OATUU), Joshua Ansah amesema chama hicho kitaendelea kusimamia na
kuhakikisha kinasimamia maslahi ya wafanyakazi Barani Afrika, ili kuhakikisha
usawa na maslahi kwa wafanyakazi wote.
Aidha, ameshukuru viongozi wa vyama vya Wafanyakazi Afrika
kwa kuendelea kuunga Mkono Shirikisho hilo katika kufanikisha jitihada za
kupigania maslahi ya wafanyakazi.
"Tuendelee kuunga mkono Shirikisho letu kwa Maslahi
mapana ya wafanyakazi barani Afrika na pamoja tutaendelea kusimamia na
kupigania kuboresha maslahi yao."
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la wafanyakazi
Kanda ya Afrika Mashariki (ILO) Bi. Caroline Mugala, Amesema Chama hicho
kitaendelea kusimamia umadhubuti na ufanisi wa vyama vya wafanyakazi ili
kuhakikisha Serikali zinaendelea kusimamia maslahi ya wafanyakazi.
"Tunahitaji kuendelea kuwalinda wafanyakazi wetu
kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kijamii ikiwemo mazingira na teknolojia ni
muhimu wafanyakazi waendelee kupewa mafunzo na kuwezeshwa kukabiliana na
mabadiriko haya."
Amesema ni lazima kila mabadiriko yanayowahusu wafanyakazi
yawahusishe wafanyakazi hao na wakubaliane nayo ili kuwa na manufaa kwa pande
zote mbili.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Tumaini
Nyamhokya, amesema chama hicho kinajivunia mafanikio makubwa ambayo kimeyapata
kwa kupigania haki za wafanyakazi wote Nchini.
Amesema mafanikio hayo yametokana na mahusiano mazuri ambayo
chama hicho kimeyajenga na Serikali pamoja na watumishi jambo ambalo
limewezesha chama hicho kufikia malengo yake na kufanya kazi kwa ufanisi.
"Tumetumia kwa kiasi kikubwa njia ya majadiliano na
maridhiano katika kufanikish mahitaji ya wafanyakazi tunashukuru kwa Upande
wetu Serikali yetu imekuwa sikuvu kusikiliza na kutatua changamoto zinazo
wakuta wafanyakazi.
Amesema chama hicho kimefurahia kuwa sehemu ya mafanikio na
kuhost mkutano Mkuu wa vyama vya wafanyakazi Afrika.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Afrika OATUU lilianzishwa mwaka Aprili 1973 na Rais wa Kwanza wa Tanzania Julius Kambarage Nyerere na Rais wa kwanza wa Ghana Fransis Kwame Nkuruma kwa lengo la kuwaunganisha wafanyakazi na kusimamia maslahi ya wafanyakazi Barani Afrika kwa pamoja.
0 Maoni