Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko, amewataka watumishi katika Wizara ya Nishati na Taasisi zilizochini ya
wizara hiyo kuwa mfano katika matumizi ya
Nishati Safi ya kupikia ili kuitekeleza kwa vitendo ajenda iliyoasisiswa
na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan
inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama kwa afya.
Dkt. Biteko ametoa maelekezo hayo tarehe 22 Agosti 2025
jijini Dodoma wakati akigawa majiko yanayotumia umeme kidogo kwa watumishi wa
Wizara ya Nishati na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo amewataka Watumishi
hao wawe mabalozi katika kutekeleza ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia.
" Leo tunagawa majiko haya kwa kuwa nyinyi ndiyo wenye dhamana kuu ya kutekeleza
Ajenda ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia hivyo wajibu wenu ni mabalozi
wazuri kwa watu wanaowazunguka ili nao wahamasike kutumia nishati hii
safi," amesema Dkt. Biteko
Amesema kufuatia mwamko mkubwa unaoendelea sasa kwa wananchi
kufahamu faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia, kiwango cha watumiaji
kimepanda kutoka asilimia 6 na kufikia
asilimia 20.3 huku lengo likiwa ni
kufikia asilimia 80 ifikapo 2034.
Dkt. Biteko ametanabaisha kuwa Idadi ya watu wanaoendelea
kutumia nishati isiyo safi na salama ya kupikia
bado ni kubwa duniani, barani
Afrika na hapa Tanzania hivyo ni jukumu la
watumishi wote wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kuhakikisha watanzania wanapata elimu sahihi
ili waweze kubadilika na kufikia lengo lililokusudiwa.
Akigawa majiko 220
kwa watumishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Biteko amepongeza Taasisi hiyo kwa kuendelea
kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya
kupikia hususan katika maeneo ya vijijini ambapo kumeonekana kuwa bado
changamoto ya kufikiwa na Nishati Safi ya Kupikia.
Pia ameipongeza REA kwa kuhakikisha Vijiji vyote 12,318 nchini vinafikiwa na
umeme.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi
Felchesmi Mramba amemhakikisha Dkt.
Biteko kuwa atakahikisha agizo alilolitoa linatekezwa na Taasisi zote
anazozisimamia.
Amesema atahakikisha
kwamba Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia
yanafikia malengo yaliyokusudiwa.
Amewasisitiza watumishi kutumia Majiko hayo waliyopewa na si kuyahifadhi.
0 Maoni