Ushirikishwaji wa vikundi vya kijamii katika matengenezo
madogomadogo ya miundombinu ya barabara umetajwa kuwa suluhisho la kupunguza
gharama kwa serikali na kuongeza uimara wa barabara nchini.
Mhandisi Ephrahim Kalunde kutoka mradi wa RISE-TARURA
ameyasema hayo wakati wa mafunzo elekezi kwa vikundi 30 vya kijamii vya
wilayani Korogwe mkoani Tanga vinavyojihusisha na matengenezo ya barabara.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo yanatolewa kupitia mradi wa
Uboreshaji Barabara Vijijini na Ufunguaji wa Fursa za Kijamii na Kiuchumi
(RISE), ambao pamoja na mambo mengine unahamasisha wananchi kushiriki katika
matengenezo madogomadogo ya barabara pindi uharibifu unapotokea.
“Njia ya kutumia vikundi kufanya matengenezo ya barabara
kwenye maeneo yao itasaidia serikali kupunguza gharama kwani matengenezo
yatafanyika kwa wakati. Pia, itapunguza gharama za kumpata mkandarasi kwa kuwa
shughuli hizi zinaweza kufanywa na wananchi waliopo kwenye eneo husika na
kuhakikisha barabara zinapitika muda wote,” amesema Mhandisi Kalunde.
Ametaja baadhi ya kazi zitakazofanywa na vikundi hivyo kuwa
ni pamoja na kukata nyasi, kusafisha mifereji ya barabara na kujenga
miundombinu midogo midogo isiyohitaji vifaa vikubwa vya ujenzi.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kalunde, kupitia mradi huo watafikia
mikoa 25 ya Tanzania Bara na kwa awamu
ya kwanza ambayo imeanza inahusisha mikoa minne na halmashauri za wilaya nane.
Naye, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka TARURA, Bw. Owigo Phinias amesema mafunzo hayo yatawajengea vikundi ujuzi wa kitaalamu hatua ambayo pia itawasaidia kujikwamua kiuchumi kupitia kazi za matengenezo ya barabara.
0 Maoni