WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa,
ametoa wito kwa wazazi na walezi kote nchini kuhakikisha wanawapeleka vijana
wao kupata mafunzo ya ufundi stadi yanayoratibiwa na Chuo cha Ufundi Stadi
(VETA) pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwawezesha kupata ujuzi utakaowasaidia
kujiajiri na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Akizungumza mara baada ya kukagua karakana za kujifunzia zilizopo katika
Chuo cha VETA wilayani Ruangwa mkoani Lindi, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa
Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha miundombinu ya vyuo vya
ufundi stadi pamoja na kuratibu programu za mafunzo ili kuhakikisha vijana
wanapata stadi zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na baadaye.
“Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha vijana wa Kitanzania
wanakuwa na ujuzi. Mafunzo ya VETA na yale yanayotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
yanawawezesha vijana wetu kuajiriwa au kujiajiri wenyewe, na hii ni hatua kubwa
ya maendeleo kwa familia zao na Taifa kwa ujumla,” alisema Waziri Mkuu.
Katika mazungumzo yake na baadhi ya wanafunzi alipokuwa akitembelea
karakana chuoni hapo, Mheshimiwa Majaliwa alifurahishwa na namna ambavyo
programu hizo za mafunzo zimekuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wanafunzi
hao.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Mohamed Salum alisema kuwa VETA
Ruangwa inaendelea kufanya maboresho mbalimbali kwa lengo la kupanua wigo wa
kozi zinazotolewa ili kwenda sambamba na mahitaji ya soko la ajira. Alitaja
jitihada zinazofanyika kuwa ni pamoja na mpango wa uanzishwaji wa fani mpya na
uwekezaji katika vifaa vya kisasa vya kufundishia.
Naye Mwanafuzi mnufaika wa programu ya mafunzo ya Ofisi wa Waziri Mkuu
Maganga Salum amesema kuwa kabla ya kujiunga chuoni hapo hakuwa na ujuzi
wowote, lakini kupitia mafunzo hayo sasa anaweza kufanya kazi za ufundi na ana
matumaini makubwa ya kujiajiri mara baada ya kuhitimu. “Tumeiva na sasa tupo
tayari kwenda kufanya kazi.”
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu pia alitembelea eneo linalojengwa hosteli
kwa ajili ya timu ya mpira wa miguu ya Namungo sambamba na kukagua uwanja wa michezo
wa Kassim Majaliwa uliopo Ruangwa ambao unatarajiwa kuwekwa viti katika
majukwa.
0 Maoni