Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) imeendelea kuimarisha
utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi wa taasisi hiyo kupitia mafunzo ya
kijeshi yanayotolewa katika kituo cha mafunzo ya kijeshi (Paramilitary)
kilichopo Mbulumbulu, Wilaya ya Karatu Mkoani
Arusha.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishina wa Uhifadhi NCAA, Katika hafla ya kuhitimisha mafunzo kwa watumishi iliyofanyika kituoni hapo leo Agusti 6, 2025, Kamishina Msaidizi Mwandamizi Victoria Shayo
alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa
jitihada zinazofanywa na NCAA kuhakikisha kwamba maafisa na askari wanapatiwa
mafunzo ili kuongeza tija katika utendaji.
“Leo tunahitimisha mafunzo kwa
Maafisa na Askari, tunaamini mafunzo
mliyopata yamewawezesha kujua mbinu na maarifa yatakayoimarisha utendaji wenu
katika kuwajengea ujasiri, ukakamavu, uweledi na utendaji kazi kwa kuzingatia
kanuni, taratibu na sheria,”alisema Victoria.
Akitoa taarifa kuhusu mafunzo hayo, mkuu wa mafunzo katika kituo hicho
Kanali Fikiri Machibya amesema kwamba mafunzo hayo yalihusisha mafunzo ya
mabadiliko ya kimuundo yanayohusisha kwata, ulengaji shabaha, masomo ya darasani pamoja na upigaji wa
buruji (Bugle) kwa maafisa na askari.
“leo tumehitimisha kozi tukiwa na jumla ya wahitimu 17 Kati ya hao wahitimu
10 walikuwa ni wa mafunzo ya mabadiliko ya muundo kozi namba tatu (3) na 7 mafunzo ya upigaji wa buruji kozi namba
moja (1)” Alisema Kanali Machibya.
Kanali Machibya, alisisitiza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwafundisha
na kuwafanya maafisa na askari kuwa wazalendo na wachapa kazi kwa ajili ya
ulinzi na Uhifadhi wa rasilimali za nchi pamoja na kuwaandaa askari kukamilisha itifaki
mbalimbali za kijeshi katika utendaji kazi wao.
0 Maoni