Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua Kampeni ya Elimu ya Kodi kwa
Biashara za Mtandaoni kwa lengo la kuhakikisha kila anayehusika na biashara
hizo anajisajili ili aanze kulipa Kodi.
Akizindua kampeni hiyo jana tarehe 09.08.2025 Jijini Dar es Salaam Kamishna
Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema wanaolengwa katika usajili huo ni
Wafanyabiashara wenye kipato cha zaidi ya Sh. Milioni 4 kwa mwaka ambao Kodi
yao itakuwa Sh. 100,000 kwa mwaka na kila mmoja atalipa kulingana na kipato
chake.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema wakati wakiendelea kutoa Elimu kwa
Wafanyabiashara wote wanaofanya biashara za mtandaoni kujisajili, wataanza na
wanaofanya biashara ya kukodisha nyumba mtandaoni pamoja na wale wanaoendesha
biashara mtao ambao wamekuwa wakipata fedha nyingi na hawalipi Kodi.
Amesema TRA itatoa asilimia 3 ya Kodi itakayookolewa kwa watu watakaotoa
taarifa za ukwepaji wa Kodi kwa Wafanyabiashara watakaoshindwa kujisajili ndani
ya muda uliowekwa na kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za wanaokwepa Kodi na
watawatambua kwa kutokutoa risiti.
"Kila anayestahili kulipa Kodi atalipa kulingana na uwezo wake na
mtaji wake na tupo kwaajili ya kuwezesha biashara hivyo hakuna mtu atakayeonewa
katika utozaji wa Kodi" amesema
Mwenda.
Amesema ili kuwezesha biashara wanaanzisha kitengo cha kuwezesha biashara
katika kila mkoa wa Kodi kitakachosaidia kurahisisha ufanyaji wa biashara na
kutatua changamoto za Walipakodi ili kuwawezesha kulipa Kodi kwa hiari.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema ili kuhamasisha matumizi ya mtandaoni TRA
imepunguza viwango vya VAT kutoka asilimia 18 mpaka 16 kwa Walipakodi
watakaofanya malipo kupitia Mtandaoni na utekelezaji wa jambo hilo utaanza
September Mosi mwaka huu.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) Dkt.
Kedmon Mapana amesema hivi sasa mifumo ya BASATA inasomana na mifumo ya TRA
Hali ambayo imerahisisha utoaji huduma na usajili wa wasanii na kazi za Sanaa
na kurahisisha ulipaji wa Kodi kwa hiari.
Mwakilishi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. John Daffa
amesema wao ndiyo wasajili wa mitandaoni yote na Kampuni zinazoendesha shughuli
za Mawasiliano nchini hivyo watashirikiana na TRA kuhakikisha ulipaji Kodi kwa
Biashara za Mtandaoni unafanikiwa.
Amesema kila mtanzania anapaswa kuona fahari kulipa Kodi kwa hiari ili
kuchangia maendeleo ya Taifa.

0 Maoni