TCRA kutoa mafunzo kwa TBN kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

 

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeandaa mafunzo maalumu kwa Mtandao wa Mabloga  Tanzania (TBN) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mafunzo haya yatafanyika kesho Jumatatu, Agosti 11, 2025, katika Makao Makuu ya TCRA.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TCRA mafunzo hayo yana lengo la kuwaandaa mabloga na wanahabari kwa ujumla ili waweze kuripoti habari za uchaguzi kwa weledi, usahihi na kuzingatia maslahi ya taifa.

Mada mbalimbali zitakazowasilishwa na wataalamu kutoka taasisi tofauti. Baadhi ya mada zitakazojadiliwa ni pamoja na Mwongozo wa Waandishi wa Habari katika Uandishi wa Habari za Uchaguzi, Kanuni za Utangazaji wa Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa za Mwaka 2020, na uhusiano kati ya Waandishi wa Habari na Jeshi la Polisi katika kulinda usalama.

Mada nyingine zitatoka Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, itakayozungumzia maadili na sheria kwa waandishi wa habari, mada kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii na Akili Unde  (AI) kuelekea uchaguzi na mada kutoka Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) itakayozungumzia Ulinzi wa Taarifa Binafsi kuelekea uchaguzi mkuu.

Mafunzo haya yana faida kubwa kwa mabloga na jamii kwa ujumla kwani yatawawezesha wanahabari kutoa taarifa sahihi na zenye uwajibikaji, jambo ambalo ni muhimu katika kujenga mazingira ya uchaguzi yenye amani na utulivu.

Pia, yanatoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na Akili Unde ili kuepuka taarifa za uongo.

Chapisha Maoni

0 Maoni