TRA yatekeleza ombi la Wahariri yaondoa VAT kwa magazeti

 

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetekeleza ombi lililotolewa mwaka jana na Wahariri kwenye mkutano wake na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) la kufutwa kwa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa magazeti, kutokana na ugumu wa biashara ya uuzaji wa magazeti.

Hayo yameelezwa na Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Juma Mwenda katika Semina ya Kutoa Elimu ya Kodi na Kuwawezesha Wafanyabishara wa Mtandaoni iliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa wafanyabiashara, mabenki pamoja na wahariri wa vyombo vya habari nchini.

“Tulipo kutana mlizungumzia kuwa Sheria ya VAT ni ngumu mtu anatoaje VAT, anauzaje magazeti lakini leo ninayo furaha ya kusema kuwa Sheria ya VAT kwa magazeti imefutwa katika kurahisisha shughuli zenu za utoaji wa habari, na hii ni ishara Mhe. Rais Samia anasikiliza ,” alisema Bw. Mwenda.

Pia, mlisema TRA tunatumia vibaya mamlaka yetu, Sheria zimetupa mamlaka makubwa lakini tunapaswa kuyatumia kwa busara (reasonable), “ Sheria za kodi zimetupa mamlaka kwa kuwa kodi ndio uhai wa taifa hivyo kama kunawatu wanakaidi kulipa kodi sheria zimetupa nguvu lakini lazima zitumike kwa hekima.”

Amesema kiutawala pamoja ya kwamba bado TRA wana mamlaka makubwa lakini watayatumia kwa usawa (fairly), kwa mwendelezo (consistently) na kwa uangalifu (carefully), “Napenda kuwaambia wafanyabiashara kuwa tutaendelea kutumia mamlaka tuliyonayo fairly, consistently and carefully.”

Amesema kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania itaendelea kusikiliza yale yote ambayo wadau wake na wafanyabiashara wanawaambia na wakiona yanatija watashauri kwa sababu kwa mujibu wa sheria TRA ni washauri wakuu wa masuala ya sheria.


Chapisha Maoni

0 Maoni