Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)
imebaini kuwepo kwa bidhaa bandia za maji ya Dettol zenye ujazo wa mililita 50,
125, 500 pamoja na lita moja, ambazo zimekuwa zikiuzwa katika soko la ndani
kinyume na sheria.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo
na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, bidhaa hizo zimegundulika kupitia mifumo ya ukaguzi
na ufuatiliaji wa bidhaa sokoni, na zimekuwa zikitengenezwa kwa njia isiyo
halali huku zikiwa zimebandikwa lebo za kuonesha kuwa ni Dettol halisi.
TMDA imeeleza kuwa utengenezaji wa
bidhaa hizo bandia ulibainika kufuatia taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa
na mamlaka hiyo, na baadaye kufuatiwa na ukaguzi uliofanyika kwa kushirikiana
na Jeshi la Polisi katika nyumba ya wageni ya New Kashinde Lodge iliyopo Mtaa
wa Namanga, Kahama Mjini, mkoani Shinyanga.
Katika ukaguzi huo, walikuta vifaa
mbalimbali vya kutengenezea bidhaa hizo ikiwa ni pamoja na kemikali, chupa tupu
za Dettol, lebo, rangi, pamoja na madumu ya vimiminika. Vitu hivyo vilikuwa
ndani ya chumba walichokuwa wanaishi raia wawili wa nchi jirani, ambao
wanatuhumiwa kuhusika na tukio hilo.
Mamlaka hiyo imethibitisha kuwa
watuhumiwa hao wamekamatwa na kufikishwa katika vyombo vya usalama, huku
taratibu za kisheria za kuwafikisha mahakamani zikiendelea.
TMDA imetoa wito kwa wananchi kuwa
makini na bidhaa wanazonunua sokoni, na kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo
watabaini bidhaa zenye mashaka.
0 Maoni