Mfuko wa SELF (SELF Microfinance Fund)
umefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 196.9 katika kipindi
cha kuanzia mwaka 2021 hadi kufikia Juni 30, 2025, huku kiwango cha mikopo
chechefu kikiripotiwa kuwa chini ya asilimia 10 na mfuko huo ukiweza
kujiendesha kwa faida.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
uongozi wa mfuko huo jana kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari, jumla ya wanufaika
183,381 wamefikiwa na mikopo hiyo, ambapo wanawake walikuwa 97,170 sawa na
asilimia 53 na wanaume 86,211 wakichangia asilimia 47 ya wanufaika wote.
Katika kipindi hicho, SELF pia
imefanikiwa kuzikopesha na kuzijengea uwezo taasisi ndogo za fedha 549, hatua
inayolenga kuboresha huduma na ufanisi katika sekta ya huduma ndogo za kifedha
nchini.
“Kuziwezesha taasisi hizi kwa maarifa
na mbinu bora za uendeshaji kumechangia kupunguza changamoto mbalimbali katika
utoaji wa huduma kwa jamii,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, mfuko huo umechangia kwa kiasi
kikubwa katika uundaji wa ajira, ambapo zaidi ya nafasi 183,000 za ajira
zimeripotiwa kutengenezwa kupitia wakopaji na shughuli wanazozifanya kuanzia
mwaka 2021 hadi Juni 2025.
Katika jitihada za kuchochea maendeleo
endelevu na kulinda mazingira, SELF imeanza pia kutoa mikopo kwa ajili ya
upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa
kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa kaya mbalimbali.
Mbali na hayo, SELF imeendesha mafunzo
ya elimu ya fedha kwa wananchi 10,378 katika kipindi hicho, ikiwa ni mkakati wa
kuinua uelewa wa jamii kuhusu masuala ya kifedha, usimamizi wa mikopo na
ujasiriamali.
0 Maoni