WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo
(Jumamosi, Agosti 16, 2025) ameshiriki uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa
reli ya kisasa ya kutoka Uvinza hadi Musongati na kuwahahikishia Watanzania na
WanaBurundi kwamba ujenzi huo utaanza katika muda uliopangwa.
Waziri Mkuu ambaye ameshiriki hafla
hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema reli hiyo itakayokuwa
na urefu wa km.240 pindi ikikamilika,
itakuwa ndiyo reli ya kwanza inayounganisha nchi na nchi katika ukanda wa
Afrika Mashariki.
Akizungumza katika hafla hiyo
iliyofanyika eneo la Musongati, Burundi,
Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo kutasaidia
kuunganisha masoko na kuendeleza biashara baina ya Tanzania na Burundi.
"Reli ikikamilika itafungua fursa
kwa wananchi wetu ambao wataweza kutoka hapa hadi Dar es Salaam ndani ya siku
moja. Hata kwenye usafirishaji wa mizigo, hivi sasa, lori linatumia saa 96
kutoka Dar hadi Bujumbura lakini baada ya kukamilisha ujenzi, usafirishaji wa
mizigo kwa kutumia treni utatumia saa 20 tu."
"Mradi wa reli ya kisasa siyo tu
kwamba utarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, bali pia utafungua
milango ya fursa mpya za uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na
Burundi."
Akielezea kuhusu mradi huo, Waziri
Mkuu amesema ujenzi wa reli hiyo utagharimu dola za Marekani bilioni 2.154 na
unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitano na
kwamba mwaka mmoja baada ya ujenzi utakuwa ni wa matazamio.
Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Meja Jenerali Evarist Ndayishimiye alisema
kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo kutatibu shauku ya muda mrefu ya nchi hiyo kuwa
na usafiri wa reli.
"Leo ni siku ya furaha sana
kwetu. Tumepata jawabu la tangu enzi na enzi. Mwaka 1921, mradi huu ulianzishwa
na Wabelgiji kisha wakaja Wajerumani lakini wakashindwa. Leo hii Tanzania na
Burundi tumeweza," alisema.
Alisema nchi yake imebarikiwa kuwa
madini mengi na kuna wakati aliitisha kikao cha wawekezaji kutoka nchi kadhaa.
"Wengi walivutiwa na wakataka kuwekeza mara moja, lakini wakaniuliza,
tukianza kuchimba madini ya Nickel, tutayasafirishaje?"
"Hiyo changamoto ilitufanya
tubungue bongo zetu na kutafuta suluhisho.
Tunaishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa kukubali kuungana nasi ili
tuanze mradi huu muhimu. Tukitoka hapa, tunataka reli iunganishe hadi Kindu,
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Na baada ya hapo, tunataka
reli yetu ifike Afrika Magharibi kwenye ufukwe wa bahari ya Atlantiki kwani
tunaamini njia hiyo itaharakisha kuleta maendeleo."
Rais Ndayishimiye alimpongeza Rais
Dkt. Samia kwa kufikia hatua kubwa za maendeleo. "Ukirudi nyumbani mwambie
Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwamba tunampongeza sana kwa kuleta
maendeleo ya haraka nchini Tanzania."
"Nimekaa Tanzania kwa muda mrefu
lakini kwa sasa nikija naweza kupotea. Magomeni napajua, Tabata na Vingunguti
napajua, Mwenge napajua, na Kinondoni nilishakaa; lakini kwa sababu ya
maendeleo yaliyopatikana, naweza kupotea. Tunamshukuru kwa uongozi wake
imara,"
Rais huyo alizungumza kwa Kiswahili na
kuamsha shangwe miongoni mwa wananchi waliohudhuria tukio hilo.
Mapema, Waziri wa Uchukuzi, Prof.
Makame Mbarawa alisema utekelezaji wa mradi huo unaenda sambamba na Ajenda 63
ya Umoja wa Afrika ambayo inataka bara la Afrika liunganishwe kwa mtandao wa
reli ya kisasa.
Alisema mbali na kuziunganisha nchi
hizo mbili, kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo, kutarahisisha kupunguza gharama
za usafirishaji wa mizigo. "Hivi sasa, kontena moja la futi 20
linasafirishwa kwa gharama ya dola za Marekani 3,800 lakini reli ikikamilika,
gharama itashuka hadi dola za Marekani 2,000.
Alisema faida nyingine itakayopatikana
baada ya mradi huo kukamilika ni kuwezesha kusafirisha mizigo mingi kwa wakati
mmoja. "Hivi sasa, mzigo unaosafirishwa kwa lori moja ni tani 30, lakini
reli ikianza kazi, tutaweza kusafirisha tani 3,000 kwa wakati mmoja,"
alisema Waziri Mbarawa.
0 Maoni