Wakulima wa nyuki katika Kijiji cha
Kangeme, Kata ya Ulowa, wilayani Kahama sasa wanatarajia kunufaika na ongezeko
la thamani ya mazao ya nyuki baada ya kuzinduliwa kwa kituo cha kukusanya na
kuchakata asali kilichojengwa kwa gharama ya Sh milioni 84.
Kituo hicho, chenye uwezo wa kuhifadhi
zaidi ya tani 90 za asali, kimejengwa na Shirika la Maendeleo la Ubelgiji
(Enabel) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia ufadhili wa Umoja wa
Ulaya (EU) chini ya mradi wa BEVAC.
Akizindua kituo hicho kwa niaba ya
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Frank John Mkinda
alisisitiza usimamizi makini wa mradi huo ili kuhakikisha unaleta matokeo
yaliyokusudiwa kwa wanachama na jamii kwa ujumla.
“Ninawataka viongozi wa Chama cha
Ushirika cha Wafugaji Nyuki Ulowa kuhakikisha kituo hiki kinasimamiwa vizuri na
kufikia malengo yaliyowekwa. Hii ni fursa kubwa ya kuongeza kipato kwa
wananchi,” alisema.
Vilevile, aliitaka Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) kushirikiana kwa karibu na wafugaji nyuki hao kwa
kuwajengea uwezo, kuwasaidia kuongeza tija katika uzalishaji na kuhakikisha
wanapata masoko yenye uhakika.
Mbali na hayo, alihimiza washiriki
wote kuimarisha uwezeshaji katika mavuno ya mazao yatokanayo na nyuki ili
kuongeza thamani na usalama wa kipato cha wananchi.
Mara baada ya hotuba hiyo, Mkuu wa
Wilaya alifungua kituo hicho na kukabidhi rasmi nyaraka za umiliki kwa Chama
cha Wafugaji Nyuki Ulowa, ambacho sasa kitakuwa msimamizi na mmiliki
halali wa kituo hicho.
0 Maoni