Taasisi ya The Same Quality Foundation inayopatikana Arusha,
kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Hospitali ya Lumumba ya Zanzibar,
imeendesha kambi ya upasuaji wa midomo wazi kwa watu wenye tatizo hilo, ikiwa
ni muendelezo wa huduma zinazotolewa na taasisi hiyo kwa lengo la kuhakikisha
watoto na watu wenye midomo wazi wanapatiwa matibabu.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo,
Dkt. Piter Mabula, amesema tangu waanze kushirikiana na sekta ya afya nchini
Tanzania, tayari wameweza kutoa matibabu kwa zaidi ya watu 2,500, ambapo kati
yao, 200 wamehudumiwa hapa Zanzibar.
Dkt. Mabula ameongeza kuwa kwa wiki moja, wataalamu wa
taasisi hiyo watakuwa katika Hospitali ya Lumumba wakifanya upasuaji kwa
kushirikiana na baadhi ya madaktari bingwa wa ndani ya nchi, ili kuhakikisha
huduma hiyo inawafikia wahitaji wengi zaidi.
Amesisitiza kuwa huduma hizi hazitozwi malipo yoyote, na
ametoa wito kwa jamii, hasa wazazi wa watoto wenye tatizo la midomo wazi,
kuwafikisha hospitalini mapema ili waweze kupata matibabu. Ameeleza kuwa
taasisi yao imejipanga kusaidia jamii na kuondoa changamoto ya tatizo hilo kwa
watoto na watu wazima.
Aidha, Dkt. Mabula ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kupitia Wizara ya Afya kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika
miaka 11 ya utekelezaji wa huduma hizi kwenye hospitali mbalimbali za Unguja na
Pemba, zikiwemo Hospitali ya Abdalla Mzee mkoani na Mnazi Mmoja.
Kwa upande wake, Daktari wa kinywa na meno kutoka Hospitali
ya Lumumba, Dkt. Sumaiyya Said Aboud, amesema kambi hizo ni endelevu na
hufanyika mara mbili kwa mwaka, ambapo kwa sasa wanatarajia kufanya upasuaji
kwa watoto 25. Amesisitiza kuwa wazazi wawapeleke watoto hospitalini mapema ili
wapate huduma na kuishi maisha ya kawaida.
Ameeleza kuwa tatizo la midomo wazi linaweza kuondolewa
kabisa kupitia upasuaji, na kwamba linapomkumba mtoto huathiri muonekano wake,
uwezo wa kula, na hata kuzungumza. Hivyo, amewataka wazazi kuwa na mwitikio wa
haraka kufikisha watoto wao hospitalini ili wapewe matibabu.
Naye Bi Leyla Saidi, mzazi wa mtoto aliyefika hospitalini
kwa ajili ya matibabu, amesema mtoto wake anaendelea vizuri na sasa anaweza
kuzungumza kwa ufasaha. Amewahamasisha wazazi wenye watoto wenye matatizo kama
hayo kupeleka watoto wao hospitalini kwa kuwa huduma hutolewa kwa weledi na
bila usumbufu wowote.
Wananchi waliopatiwa huduma na taasisi hiyo wamesema
wamefurahishwa na huduma bora walizopokea na wameipongeza taasisi kwa moyo wa
kutoa misaada ya afya, wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kuunga mkono juhudi
hizo kwa ustawi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
The Same Quality Foundation inaendelea kutoa huduma mbalimbali za afya kwa jamii ya Tanzania Bara na Zanzibar, kwa kuwalenga hasa watoto na watu wazima wenye matatizo ya midomo wazi. Kwa sasa, huduma hizo zinaendelea kutolewa hapa Zanzibar kwa muda wa wiki moja.
0 Maoni