Korea Kusini yapiga marufuku matumizi ya simu shuleni

 

Korea Kusini imekuwa nchi ya hivi karibuni kuzuia matumizi ya simu miongoni mwa watoto na vijana baada ya kupitisha muswada unaopiga marufuku matumizi ya simu za mkononi na vifaa vingine vya kisasa vya kielektroniki wakati wa saa za darasani katika shule.

Sheria hiyo, itakayoanza kutekelezwa kuanzia mwaka mpya wa shule mwezi Machi 2026, ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya pande mbili za kisiasa ili kukabiliana na uraibu wa simu janja, huku tafiti zikionyesha athari zake mbaya.

Wabunge, wazazi na walimu wanasema kuwa matumizi ya simu yanaharibu utendaji wa kitaaluma wa wanafunzi na kuchukua muda ambao wangeweza kuutumia kusoma.

Hata hivyo, marufuku hiyo ina wakosoaji wake, wakiwemo baadhi ya wanafunzi, ambao wanahoji  jinsi itakavyotekelezwa, athari zake kwa upana zaidi, na iwapo kweli inashughulikia chanzo halisi cha uraibu huo.

Muswada huo ulipitishwa kwa kishindo alasiri ya Jumatano, kwa kura 115 za kuunga mkono kati ya wabunge 163 waliokuwepo.

Shule nyingi za Korea Kusini tayari zimeweka aina fulani ya marufuku ya simu. Na si wa kwanza kufanya hivyo.

Baadhi ya nchi kama Finland na Ufaransa zimepiga marufuku simu kwa kiwango kidogo, kwa kuzuia tu katika shule za watoto wadogo. Nchi nyingine kama Italia, Uholanzi na China zimepiga marufuku matumizi ya simu katika shule zote.

Chapisha Maoni

0 Maoni