Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshiriki hafla ya ufunguzi
wa Mkutano wa Tano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Singapore
(SAMEV), uliofanyika tarehe 26 Agosti 2025 jijini Singapore.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit
Kombo.
Akifungua mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore,
Mhe. Dkt. Vivian Balakrishnan, alibainisha kuwa Mkutano huo unajadili mbinu za
kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, uchumi na maendeleo endelevu kati ya
Singapore na nchi za Afrika. Alisisitiza kuwa ushirikiano huo unapaswa kuwa
nguzo ya pamoja kukabiliana na changamoto mpya za uchumi na biashara duniani.
“Tunaishi katika nyakati zenye misukosuko mikubwa
inayosababisha kudorora kwa ukuaji wa uchumi na biashara duniani. Vikwazo vya
kibiashara, mabadiliko ya sera, ongezeko la ushuru usio wa kawaida, majanga ya
asili na migogoro ya kisiasa vimeathiri kwa kiasi kikubwa mfumo wa uchumi wa
kimataifa. Huu ni wakati muafaka wa kuweka mikakati ya pamoja ili tuweze
kuhimili changamoto hizi na kuendelea kukua kiuchumi,” alisema Dkt. Balakrishnan.
Katika hotuba yake, Dkt. Balakrishnan alitaja maeneo ya
kimkakati ambayo yataimarishwa kupitia ushirikiano wa Afrika na Singapore, na
ambayo Tanzania itanufaika nayo moja kwa moja kuwa ni Fursa za masoko ya bidhaa
za kilimo na madini zinazozalishwa nchini, Uwekezaji katika teknolojia na
nishati jadidifu, Ufadhili wa masomo na mafunzo ya ufundi kwa vijana, Mapambano
dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, Ukuaji wa uchumi wa kidijitali na uchumi wa
buluu na Uwekezaji katika sekta ya viwanda na biashara.
Aidha, Waziri Balakrishnan alieleza kuwa Singapore imeamua
kuimarisha uhusiano wake na Afrika kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi
na kisiasa duniani, hali inayohitaji mshikamano wa kimataifa. Alisisitiza kuwa
Afrika na Asia ya Kusini-Mashariki zina nafasi ya kipekee ya kushirikiana kwa
kuzingatia rasilimali tele, ukuaji wa kasi wa idadi ya watu, na ukubwa wa
masoko.
Akiainisha sababu zinazovutia Singapore kuelekeza mikakati
ya maendeleo Afrika, alibainisha mambo kadhaa muhimu ikiwemo idadi kubwa ya watu
barani Afrika (takribani bilioni 1.3), ardhi kubwa na yenye rutuba, nafasi
nzuri ya kijiografia, nguvu kazi yenye vijana walio chini ya miaka 30
wanaokaribia asilimia 70 ya idadi ya watu, hali ya amani na usalama, kasi ya
ukuaji wa uchumi, na upatikanaji wa malighafi.
Vilevile, alitambua juhudi za nchi za Afrika katika kujenga
uchumi wake kupitia utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA)
pamoja na uwepo wa Jumuiya za Kikanda za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Alibainisha kuwa Singapore iko tayari kushirikiana na
jumuiya hizo kwa njia zitakazokubaliwa ili kuongeza kasi ya maendeleo kwa pande
zote mbili.
Mkutano wa SAMEV hufanyika kila baada ya miaka miwili, ambapo kwa mara ya kwanza ulifanyika mwaka 2014. Ufunguzi wa mkutano wa mwaka huu pia ulihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Ghana, Mhe. John Dramani Mahama.



0 Maoni