Taifa Stars wapewa viwanja na milioni 20 ikiivaa Morocco leo

 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, imejipanga kwa dhati kuendeleza michezo nchini kwa kuweka mazingira bora ya mafanikio kwa vijana.

Akizungumza leo Agosti 22, 2025 jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mchezo wa kuwania kufuzu CHAN kati ya Taifa Stars na Morocco, Mhe. Chalamila alibainisha kuwa Rais Samia ameidhinisha zawadi ya viwanja kwa wachezaji wa Taifa Stars katika eneo la Kigamboni pamoja na shilingi milioni 20 taslimu, kama sehemu ya kutambua mchango wao kwa taifa.

“Hii zawadi ya viwanja na shilingi milioni ishirini haitahusishwa na matokeo ya mchezo. Iwe tumeshinda au tumepoteza, vijana wetu wa Taifa Stars watapata zawadi hizi kwa kutambua mchango wao na kuwatia moyo zaidi,” alisema Chalamila.

Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza kuwa serikali imejipanga kuhamasisha na kuwaunga mkono vijana wanaoiwakilisha nchi katika ngazi ya kimataifa, akieleza kuwa kwa kila bao litakalofungwa na Taifa Stars kwenye mchezo huo, serikali itatoa motisha ya shilingi milioni tano.

“Kila goli litakaloingia wavuni kutoka kwa vijana wetu wa Taifa Stars, serikali itachangia shilingi milioni tano kama sehemu ya kuwatia moyo,” alisema.

Kwa mujibu wa Chalamila, hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kuongeza morali kwa wachezaji na kuonyesha mshikamano wa dhati kati ya serikali, wananchi na timu ya taifa katika mashindano ya kimataifa.

“Hii ni sehemu ya mikakati ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha michezo inakuwa na vijana wetu wanathaminiwa ipasavyo. Tunatoa rai kwa wadau wa michezo kujitokeza na kuunga mkono jitihada hizi za kuinua soka letu,” aliongeza Chalamila.

Mchezo huo ni sehemu ya hatua muhimu kwa Tanzania kuelekea kushiriki michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN), na serikali imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya michezo ili kufikia mafanikio ya muda mrefu.

Chapisha Maoni

0 Maoni