Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kuwezesha, kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa watumishi na askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (2024 – 2034).
Hayo yamebainishwa jana Agosti 11, 2025 na Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala
wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Kanali Juma Mrai
wakati akifungua mafunzo kwa washiriki toka vikosi 22 vinavyonufaika na mpango wa nishati safi
JKT katika bwalo la vijana 834KJ (Makutupora) jijini Dodoma
"Hii yote ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jumhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu taasisi zote zinazohudumia
watu zaidi ya 100 zihame kutoka katika matumizi ya nishati chafu na kuhamia katika
nishati safi ya kupikia, " ameongeza Kanali Mrai.
Aidha, ameipongeza REA kwa kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya nishati safi ili kutunza
mazingira na kuepuka athari za kiafya zinazohusiana na utegemezi mkubwa wa
nishati isiyo kuwa safi.
"REA imeiwezesha JKT kwa asilimia 76 Sawa na Shilingi Bilioni 4.37
ya utekelezaji wa nishati safi katika kambi 22 za JKT kwa kuzipatia mashine za
kutengeneza mkaa Mbadala 60, majiko banifu 291, mifumo ya gesi ya LPG 180 na
masufuria yake, Mkaa Mbadala tani 220, mafunzo kwa vijana 50,000 pamoja na
mifumo ya Gesi Vunde 9," amesisitiza Kanali Mrai.
Katika hatua nyingine, amewataka watendaji waliolengwa kutumia mashine za
kutengeneza mkaa mbadala, majiko banifu na majiko ya gesi pamoja na mkaa rafiki
wa mazingira unaotokana na mabaki ya mazao ya shambani kupatiwa elimu ili kuwa
na uwezo wa kubaini na kutatua changamoto za nishati hiyo na hatimaye bidhaa
hizo kuleta tija kwa taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala
kutoka REA, Mha. Advera Mwijage amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo
maafisa na askari wa vikosi vilivyopo katika mpango wa REA ili waweze kuwa
mabalozi wazuri wa matumizi ya nishati
safi ya kupikia kwenye maeneo yao ya kazi.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatachangia katika mlolongo mzima wa kuwa na
matumizi endelevu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa sababu mafunzo haya yanatoa
fursa ya kupata ujuzi utaowawezesha Kusimamia mifumo ya Nishati safi vizuri.
Pia, amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa kwa utekelezaji mzuri wa mradi
na kuahidi ushirikiano katika kuhakikisha tunakamilisha mradi huu kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Mha. Mwijage amebainisha kuwa, tayari REA
imeidhinisha zaidi ya milioni 800 kwa ajili ya watumishi 7,000 wa JKT kupatiwa
Mtungi wa kilo 15 wa LPG pamoja na Jiko lake la sahani mbili kila mmoja ikiwa ni sehemu wa kuhamasisha matumizi ya
Nishati safi ya Kupikia kwa mtu mmoja mmoja.
0 Maoni