Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka waandishi wa habari
kutokuwa sehemu ya kukuza migogoro katika kipindi cha uchaguzi mkuu na kuwaasa
wajiulize kwanza habari wanayotaka kuitoa iwapo italeta athari gani kwa jamii
na kwa amani ya nchi.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Meneja Kitengo cha Huduma za
Utangazaji TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka katika mafunzo yaliyotolewa kwa Mtandao
wa Wana Blogu wa Tanzania (TBN) ambapo mada saba ziliwasilisha ili kuwajengea
uwezo mabloga kuelekea uchaguzi mkuu.
“Katika machafuko na migogoro waandishi wa habari mnapaswa kuangalia
taarifa zenu mnazochapisha na kuzitangaza ili msiwe sehemu ya kukuza migogoro
na kuhatarisha amani na utulivu,” alisema Mhandisi Kisaka.
Mhandisi Kisaka amewahimiza waandishi wa habari kuzingatia kutoa elimu kwa mpiga kura, kutoa taarifa za mwenendo wa kampeni, kutoa taaria ya nini kinaendelea wakati wa uchaguzi pamoja na kutangaza matokeo yatakayotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).
Kwa upande wao Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Engbert
Mkoko na Dkt. Darius Mukiza wakitoa mada kwa nyakati tofauti walisisiti
waandishi wa habari kuzingatia sheria mbalimbali wakati wakitekeleza majukumu
yao katika kipindi chote cha uchaguzi na kuwa makini na habari za upotoshaji.
Naye Afisa kutoka Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari-JAB, Rehema
Mpagama akiongea kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula
amewataka waandishi wa habari kuhakikisha kuwa wamepatiwa kwanza ithibati na
kupewa press card ndipo washiriki kuripoti uchaguzi mkuu.
Kwa upande wake Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano - PDPC, Innocent Mungy
amewatahadharisha waandishi wa habari kuwa katika kipindi hiki cha uchaguzi
kuna vihatarishi vingi vinavyohusiana ukiukaji wa ulinzi wa taarifa binafsi.
Awali Kaimu Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe alitoa shukrani kwa Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Katibu Mkuu wake, Ndugu Gerson Msigwa,
kwa kuona umuhimu wa TBN na kuwezesha mafunzo hayo.
Pia, aliishukuru Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuandaa na
kuratibu mafunzo haya muhimu ambayo yanalenga kutuandaa mabloga kuripoti habari
za uchaguzi kwa weledi na uadilifu.
Beda amesema kuwa kwa miaka mingi, Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) umekuwa
sauti muhimu katika jamii. “Tumekuwa jukwaa huru linalowapa Watanzania fursa ya
kutoa mawazo yao, kushiriki uzoefu, na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu
jamii yetu.”
“Jukumu letu si tu kutoa habari, bali pia kuhakikisha habari hizo ni
sahihi na zinazingatia maadili na utamaduni wa Kitanzania. Tunapaswa kulaani
vikali wale wote wanaokwenda kinyume na maadili yetu, wanaosambaza habari za
uongo na za uchochezi,” alisema Beda.
0 Maoni