Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), imetoa kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kwenye mradi wa kuzalisha
umeme wa maji Lupali wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 317 unaotekelezwa na
shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha.
Hayo yamebainishwa leo
Agosti 1, 2025 na Mjumbe wa Bodi, Bw. James Mabula wakati akizungumza kwa niaba
ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali
Mstaafu Jacob Kingu, walipotembelea mradi
wa Lupali unaotumia nguvu ya maporomoko madogo ya maji ya mto Lupali katika
kuzalisha umeme mkoani Njombe.
Amesema kuwa, fedha
zilizotolewa na REA zimewezesha ujenzi wa kituo cha uzalishaji wa umeme na
miundombinu ya usambazaji kwenye kituo cha Imiliwaha Sisters Convent pamoja na
vijiji vya jirani vya Boimanda, Kitulila na Matola sambamba na kuwezesha tafiti
za mradi huo.
"Hii ni pamoja na
gharama za utafiti wa awali wa mradi, ujenzi wa njia kuu za kusafirisha umeme
(11kV) kilomita 23.48 na njia ndogo za kusambazia umeme kwa watumiaji kilomita
30.61," Amesema Bw. Mabula.
Aidha, utekelezaji wa
mradi huo umefikia asilimia 98 ambapo kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja
na ujenzi wa kizuizi cha maji na mtaro wa kupitisha maji ya mafuriko ambao
tayari umekamilika.
Ameongeza kuwa,
wamekamilisha ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme (Powerhouse, mfereji wa
kurudisha maji mtoni pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha maji na ununuzi
wa vifaa vya umeme uliofikia asilimia 90.
Kwa upande wake, Mshauri
wa Biashara wa mradi huo, Bw. Malimi
Sitta amesema kuwa, mara baada ya mradi kukamilika, umeme utakaozalishwa
utauzwa moja kwa moja kwa TANESCO ambapo tayari mkataba wa kuuziana umeme
umeshasainiwa.
Ameongeza faida za mradi
utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi kwa
matumizi ya nyumbani na biashara na kupinguza matumizi ya nishati isiyo rafiki
na mazingira.
Ziara hiyo ya REB mkoani
Njombe imelenga kupitia utekelezaji wa
miradi ya REA inayotekelezwa katika huo sambamba na kupitia changamoto za
waendelezaji wadogo wa miradi ya kuzalisha umeme hapa nchini na kupatiwa
ufumbuzi.
0 Maoni