PSSSF yalia na waajiri wasiowasilisha makato ya wanachama

 

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeviomba vyombo vya habari kuusaidia katika kuwahamasisha waajiri kuwasilisha makato ya michango ya pensheni ya wanachama wao.

Ombi hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam na Meneja wa PSSSF kanda ya Ilala Bw. Hajji Khamis katika mkutano wa Wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), wakati akielezea mambo mbalimbali yanayotekelezwa na mfuko huo.

“Moja ya changamoto kubwa tunayokabiliana nayo kwa sasa ni waajiri kutowasilisha makato ya michango ya pensheni ya wanachama wetu kwa wakati,” alisema Bw. Khamisi na kuongeza;

“Wahariri mtusaidie kuwahamasisha waajiri kuwasilisha makato ya michango ya pensheni ya wanachama wetu, kwani kwenye makato kuna haki ya wanachama wetu.”

Kuhusu matumizi ya teknolojia amesema kwa asilimia 90 sasa michakato yote ya PSSF inafanyika kimtandao jambo ambalo limefanikisha kuboresha utoaji huduma wa mfuko huo kwa wanachama wake.

Kuhusu ulipaji wa pensheni wanachama wao kwa wakati Meneja wa PSSSF kanda ya Ilala Bi. Amina Kasim amesema PSSSF kwa sasa wamejitahidi katika kuhakikisha kuwa wanachama wanalipwa pensheni zao kwa wakati kila mwezi kuanzia kati ya tarehe 23-25.

“Kwa sasa mwanachama wetu anaweza kuhakiki taarifa zake akiwa popote halipo hata nyumbani, hakuna tena haja ya kuja ofisini kwa ajili ya kujua taarifa mbalimbali kwa mwanachama,” alisema Bi. Khadija.

Amesema na kwa wale watu wazima mno na wagonjwa ambao hawawezi kutumia teknolojia ama hawana wasaidizi wanaowaamini, wanapatiwa huduma kwa kufuatwa walipo baada ya kupiga simu PSSSF ya kuomba msaada.





Chapisha Maoni

0 Maoni