Jumla ya shilingi Milioni 148.5 zimetumika Kujenga Daraja la kinyang'erere lililopo katika
kijiji cha kinyang'erere halmashauri ya Musoma Mkoani Mara.
Akisoma Taarifa ya ujenzi wa Mradi huo
Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Musoma Mhandisi Mohmed Etanga amesema daraja
hilo limekamilika ujenzi wake kwa asilimia mia moja na kutoa huduma kwa
Wananchi kama ilivyo kusudiwa.
Mhandisi Etanga ameongeza kuwa daraja
hilo ni kiungo muhimu kwa wakazi wa kijiji hicho kwaajili ya usafirishaji wa
Mazao na kwenda kupata huduma za kijamii katika vijiji vingine ambapo kuna
kituo cha Afya pamoja na wanafunzi kuvuka kwenda shule.
Ameongeza kuwa kipindi cha Masika
wakazi hao walikuwa wakipitia kadhia ya kushindwa kuvuka mto ambao unakuwa
umejaa maji jambo lilikuwa likisababisha baadhi ya wajawazito kujifungulia
njiani na kushindwa kuuza mazao yao kutokana na ubovu wa barabara.
Naye Kiongozi wa Mbio za Mwenge
Kitaifa Ndugu Ismail Ali Ussi ameipongeza TARURA kwa kufanya kazi hiyo kwa kiwango
kinachotakiwa.
"Nichukue nafasi hii kumpongeza
Meneja wa TARURA Mkoa na timu yake kwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa," amesema Ussi.
Mbali na kutoa kongole kwa watumishi
wa TARURA amemshukuru pia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa Fedha nyingi kwa lengo la
Ujenzi wa Miradi ya maendeleo kwa wanachi katika maneno mbalimbali nchini.
Mbali na hilo Ussi amewaasa wananchi
kutunza miundombinu hiyo ili iwe endelevu kutokana na kutumia gharama nyingi
katika utengenezaji wake na endapo wataitunza itaendelea kuwa imara na kutumika
kwa kipindi kirefu zaidi.
0 Maoni