Timu ya soka ya Watanzania iitwayo
Kilimanjaro kutoka Sweden imetwaa tena kwa mara ya nne mfululizo ubingwa wa
kombe la Bonanza la Serengeti katika michuano iliyofanyika tarehe 15-16 Agosti,
2025, jijini Antwerp, Ubelgiji.
Kilimanjaro ilitetea ubingwa wake
baada ya kuifunga timu nyingine ya Watanzania kutoka Uingereza iitwayo Leeds
Swahili mabao 2-1 kwenye mchezo mkali wa fainali. Magoli ya Kilimanjaro
yalifungwa na Feisal Amir na Fryad Sabri huku la Leeds likifungwa na Murtaza
Fuad. Hii ni mara ya tatu kwa timu hizi kukutana fainali.
Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji,
Mhe. Jestas Nyamanga, alimkabidhi kombe la ubingwa nahodha wa Kilimanjaro,
Abbas Bachu, ambaye naye alimkabidhi Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe.
Mobhare Matinyi, na kuibua shwange za washabiki wao. Kilimanjaro hushiriki ligi
ya daraja la sita nchini Sweden katika mfumo wa madaraja saba.
Michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya
nne tangu mwaka 2021 na kudhaminiwa na Benki ya NBC na kampuni ya ASAS, zote za
Tanzania, huandaliwa kwa lengo la kuwaunganisha Watanzania Ughaibuni, kukuza
vipaji vya soka na kuitangaza Tanzania kimataifa. Mkurugenzi wa Diaspora kutoka
Tanzania, Salvatory Mbilinyi; Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Caroline
Chipeta; na Mabalozi wa Kenya, Sudan Kusini na Somalia nchini Ubelgiji nao
walishuhudia.
Jumla ya timu 15 za Watanzania na watu
wa Afrika Mashariki waishio barani Ulaya zilimenyana. Waandaaji Tanzania
walikuwa na timu kumi kutoka Sweden, Ubelgiji, Uholanzi, Uingereza, Scotland,
Ujerumani na Ufaransa huku Burundi ikiwa na timu tatu na moja moja kutoka
Rwanda na Somalia.
0 Maoni