Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeanzisha mpango maalumu
wa kushirikisha wanasheria katika kuimarisha usalama wa waandishi wa habari
kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, hatua inayolenga kukabiliana na
changamoto za kihistoria zinazowakumba wanahabari nyakati za uchaguzi.
Mpango huo, unaofadhiliwa na Shirika la International Media
Support (IMS), unalenga kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa waandishi wa
habari wanaokumbana na changamoto kama vile kukamatwa, kutishiwa, au
kufunguliwa mashtaka wakiwa kazini.
Akizungumza katika mafunzo ya siku moja yaliyofanyika jijini
Arusha jana, Agosti 19, 2025, Jaji mstaafu Robert Makaramba aliwataka mawakili
kuwa mstari wa mbele katika kulinda uhuru wa habari, akisisitiza kuwa waandishi
ni sehemu muhimu ya mchakato wa kidemokrasia.
Mafunzo hayo yamehusisha mawakili 20 wa haki za binadamu
waliopatiwa mafunzo na MCT kati ya mwaka 2021 hadi 2023. Wakufunzi waliwapatia
uelewa wa kina kuhusu sheria zinazogusa tasnia ya habari, zikiwemo Sheria ya
Huduma za Vyombo vya Habari na Sheria ya Makosa ya Mtandao.
"Tunahitaji kujenga mtandao imara wa wanasheria walioko
tayari kutoa msaada wa kisheria kwa wanahabari pindi wanapokumbana na madhila
kazini," alisema Jaji Makaramba.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Ukiukwaji wa Uhuru wa Vyombo vya
Habari ya MCT ya 2022, licha ya kupungua kwa matukio ya ukiukwaji wa uhuru wa
vyombo vya habari kutoka 119 mwaka 2018/19 hadi 18 mwaka 2022, hali bado si
shwari.
Kwa mwaka 2024 pekee, jumla ya matukio 27 ya ukiukwaji
yaliripotiwa huku matukio mengine 17 yakitokea kati ya Januari hadi Agosti
2025. Matukio hayo ni pamoja na kukamatwa kwa wanahabari, vitisho, utekaji
nyara, maonyo, kusimamishwa kazi na kuingiliwa kwa uhuru wa uhariri.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za MCT kujiandaa mapema kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao, ambapo waandishi wa habari mara nyingi hukumbwa na mazingira hatarishi kutokana na kazi yao ya kuripoti habari za kisiasa.
0 Maoni