Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dustan Kitandula,
amelitaka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuandaa mikakati
kabambe ya kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi ya Taifa ya
Katavi pamoja na kuvutia wawekezaji wengi zaidi, ili kusaidia kuongeza idadi ya
watalii na mapato yanayotokana na sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa Taifa.
Waziri Kitandula aliyasema hayo jana, Agosti 19, 2025,
katika ziara ya kikazi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi, ambapo aliendesha
kikao cha kimkakati na Menejimenti ya Hifadhi hiyo pamoja na kutembelea maeneo
mbalimbali yaliyoko ndani ya hifadhi kuona shughuli za utalii zinazoendelea
pamoja na fursa za uwezekezaji zinazopatika katika hifadhi hiyo.
“Katavi ni miongoni mwa hifadhi zenye vivutio vizuri sana na
adimu duniani ipo haja ya kuongeza juhudi za kuitangaza hifadhi hii ndani na
kimataifa, hatuwezi kusubiri watalii waje wenyewe tuwafuate huko walipo,
tukawaeleze uzuri na fursa zilizopo
katika Hifadhi ya Taifa Katavi” alisema Waziri Kitandula.
Waziri Kitandula aliongeza kuwa, Katavi kwa sasa ipo vizuri
katika eneo la miundombinu ya barabara, kambi za kulala wageni pamoja na
viwanja vya ndege hivyo ipo haja ya TANAPA kushirikiana kwa ukaribu na
wawekezaji ili Katavi iweze kuwa kitovu cha utalii kwa kanda ya kusini.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi, anayeshughulikia
kitengo cha Utalii na Maendeleo ya Biashara TANAPA Massana Mwishawa alisema
kuwa, TANAPA imejipanga kuanzisha mikakati mikubwa ya kuitangaza zaidi hifadhi
ya Taifa Katavi pamoja na hifadhi nyingine nchini, ili kupanua wigo wa soko la
utalii sio tu barani Afrika, bali pia katika nchi za Asia na Ulaya.
Naye, Afisa Mhifadhi Mkuu Dominick Tarimo ambaye ni Kaimu
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Katavi alisema kuwa hifadhi hiyo ni miongoni mwa
maeneo yenye wanyamapori wa kipekee kama kiboko, twiga, mbwa mwitu na wengineo,
pamoja na mandhari ya kuvutia hivyo menejimenti ya hifadhi hiyo itaendelea
kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii katika kulinda na kuhifadhi
rasilimali hizo, ili kuhakikisha Katavi inaendelea kuwa sehemu salama na ya
kuvutia kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.
Hifadhi ya Taifa Katavi ni Hifadhi iliyoanzishwa mnamo mwaka 1974 ikiwa ni hifadhi ya tano kwa ukubwa Tanzania na inapatikana katika Mkoa wa Katavi ndani ya Wilaya za Mpanda, Mlele pamoja na Tanganyika.
Na. Happiness Sam- Katavi
0 Maoni