Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa
Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam Mwinyi amesema
kuwa vijana ni nguvu ya sasa ya maendeleo ya Zanzibar, na si watu wa
kuchukuliwa kama ahadi ya kesho.
Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 10 Agosti 2025, alipofungua
Jukwaa la East Africa Youth Business and Investment Expo 2025 lililofanyika
katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Mkoa wa Kusini Unguja.
Amewahakikishia vijana kuwa Zanzibar iko tayari kuwa kitovu cha ubunifu
na uwekezaji wa vijana katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Aidha, ameshauri vijana kutumia fursa zilizopo kwa kujipanga, kuwa na
nidhamu, kuendelea kujifunza, na kushirikiana kutumia majukwaa mbalimbali kwa
hatua za kimaendeleo.
Halikadhalika, Mama Mariam Mwinyi amesema kuwa Taasisi ya ZMBF
imefanikiwa kuwawezesha jumla ya vijana 602 kupitia programu za uwezeshaji wa
kijamii na kiuchumi katika sekta ya mwani, ikiwemo kuwapatia boti zenye injini,
mafunzo, ujenzi wa miundombinu ya kukaushia mwani, uhamasishaji wa vikundi vya
kuweka na kukopa, pamoja na masoko ya kidijitali ya zao hilo.
Kwa upande mwingine, Mama Mariam Mwinyi amefafanua kuwa Serikali
itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kwa kuibua mawazo bunifu, kuwapatia
mitaji na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa unaojengwa
kwa misingi ya maendeleo jumuishi na endelevu.
0 Maoni