WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema elimu ya watu wazima
sio tu elimu ya masomo ya kawaida, bali ni zana muhimu ya maendeleo endelevu,
kwani inachangia kipato, ustawi wa kijamii, afya na ushiriki wa kiraia.
ameongeza kuwa uzoefu duniani unaonesha kwamba elimu ya watu
wazima ni chombo muhimu cha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na binafsi.
Amesema hayo leo Jumatatu (Agosti 25, 2025) alipofungua
kongamano la kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu
Wazima inayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
jijini Dar es Salaam.
“Elimu si tukio la muda bali ni safari endelevu ya kujifunza
katika maisha yote, elimu ya Watu wazima si kwa ajili ya watu wazima pekee,
bali hata kundi la vijana wanaweza kujiunga na kunufaika na program mbalimbali
za ujuzi zinazotolewa na taasisi hiyo”.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa
Serikali inatambua kwamba katika kipindi cha nusu karne iliyopita, Taasisi ya
Elimu ya Watu Wazima imepiga hatua kubwa na kutoa mchango wa kipekee katika
maendeleo ya Taifa.
“Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima imekuwa ikishauri Serikali
kwenye maeneo ya kisera na kitaalamu katika masuala ya elimu ya watu wazima na
elimu nje ya mfumo rasmi iliyosaidia kuwafikia Watanzania wengi zaidi waliokuwa
hawajapata fursa ya elimu ya msingi”.
Mheshimiwa Majaliwa ameielekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuhakikisha
wanaongeza wigo wa upatikanaji wa elimu ya watu wazima ikiwemo kuwafikia
makundi yote nchini hasa maeneo yaliyo pembezoni na yenye changamoto za kijamii
na kijiografia.
Pia, ameiagiza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kwa
kushirikiana na wadau waendelee kufanya tafiti za mara kwa mara kuhusiana na
elimu ya watu wazima ili kubaini changamoto zinazojitokeza na kuandaa suluhisho
bunifu linaloendana na mahitaji halisi ya jamii.
Naye, Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa
Taasisi ya Elimu ya Watu wazima imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa na ya
kimkakati ikiwemo mradi wa SEQUIP (Secondary Education Quality Improvement
Project) ambapo umefanikiwa kuwarejesha wasichana 13,272 katika mfumo wa elimu
katika kipindi cha miaka mitano.
Amesema kuwa mradi mwingine ni IPOSA (Integrated Programme
for Out-of School Adolescents) ambao umewezesha kuwajengea uwezo vijana 10,000
walioko nje ya mfumo rasmi katika maeneo
ya stadi za maisha, ujasiriamali na ufundi wa awali.
Kwa Upande wake Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Prof. Philipo Sanga amesema kuwa Taasisi hiyo inajivunia mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita hasa katika kuboresha mifumo ya elimu ikiwemo sera ya elimu jumuishi ambayo inagusa makundi yote pasipo ubaguzi.
0 Maoni