Ahadi ya Serikali ya kufikisha umeme wa gridi ya taifa
katika Wilaya zote za Mkoa wa Kagera imetekelezwa baada ya Serikali kusaini
mikataba ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220
kutoka Benako, Ngara hadi Kyaka wilayani Misenyi na kituo cha kupoza umeme
cha Benako cha msongo wa kilovoti 220/33, hatua inayotoa uhakika kwa Mkoa huo
sasa kupata umeme wa gridi badala ya kutegemea umeme kutoka Uganda kwa kiasi
kikubwa.
Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini kwa mikataba
hiyo jijini Dodoma tarehe 25 Agosti, 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa kuanza kutekelezwa kwa mradi huo ni
moja ya maelekezo ya Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa na kiu ya
kutekeleza ahadi ya Serikali kwa wananchi wa Kagera ya kupata umeme wa uhakika muda wote ili
kutekeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
" Kupitia mradi huu, Mkoa wa Kagera kwa mara ya kwanza
na wenyewe unaingia kwenye gridi ya Taifa hasa na hivyo kuongeza uhakika wa
upatikanaji wa umeme hususan katika Wilaya za Bukoba, Muleba, Misenyi, Karagwe,
Kyerwa na maeneo mengine ya jirani, nawahakikishia watu wa Kagera kuwa
Serikali imeshaamua mradi huu ufanyike
kwa wakati kwa miezi 24 tu," amesema
Dkt. Biteko
Dkt. Biteko amesema, Kagera ambayo mahitaji yake ya umeme
hayazidi megawati 47 baada ya muda itakuwa na uhakika mkubwa wa upatikanaji
umeme kwani kutakuwa na njia mbalimbali za kufikisha umeme mkoani humo ikiwemo Benako- Karagwe
hadi Kayaka, Nyakanazi- Biharamulo hadi
Muleba na kuna mradi mwingine mkubwa
unaotarajiwa kujengwa kutoka Ibadakuli hadi Mbarara Uganda wa kV 400.
Vilevile kuna mradi wa uzalishaji umeme wa Kakono wa megawati 87 ambao upo
katika hatua za mwisho za kutafuta Mkandarasi.
Ameongeza kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pia anaendelea
kutekeleza miradi mingine ya umeme katika maeneo mengine ikiwemo mradi wa
usafirishaji umeme wa kV 400 wa Tanzania- Zambia, mradi wa Usafirishaji umeme
wa kV 400 Chalinze-Dodoma , mradi wa usafirishaji umeme wa Mkuranga -Pwani
ambao utapeleka umeme kwa wananchi wa
Kusini, pia mradi wa usafirishaji umeme wa gridi imara wa Tunduru- Masasi-
Mahumbika ambao pia unaenda kutoa uhakika wa umeme katika mikoa ya Kusini.
" Utekelezaji wa miradi hii yote ya umeme ni kielelezo
kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaonesha njia ya kuwafikishia wananchi
umeme wa uhakika sasa kinachohitajika kwa watendaji ni kukimbia badala ya
kutembea kwani kinachotakiwa ni matokeo na siyo kusema sana," amesisitiza
Dkt. Biteko.
Pia Dkt. Biteko amewashukuru wafadhili wa mradi ambao wametoa Dola za Kimarekani takriban
milioni 105.6 ambazo ameagiza kuwa zitumike kwa usahihi ili kuwapa sababu
wafadhili wengine kuendelea kusaidia miradi mbalimbali.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameagiza TANESCO
kuhakikisha wananchi 1,014 wanaopisha mradi wanalipwa fidia yao mapema iwezekanavyo yaani kuanzia mwezi
septemba mwaka huu.
Aidha, amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,
Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi
Innocent Luoga na watendaji wa
TANESCO kwa kuendelea kusimamia
kwa umakini Sekta ya Nishati.
Vilevile, ameipongeza TANESCO kwa kuendelea kuboresha
utendaji wake na kwa kusimamia haki hasa
pale zabuni zinapotangazwa. Aidha ametaka mipango iliyowekwa kwenye mradi huo
iheshimiwe ili thamani ya fedha ionekane na wananchi wapate huduma kwa wakati.
Dkt. Biteko ameomba wananchi mkoani Kagera kuchangamkia
fursa kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika mara baada ya miradi
itakayofikisha umeme mkoani humo kukamilika.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwassa amepongeza
Serikali kwa kuona umuhimu wa kutekekeza
mradi huo wenye gharama kubwa ikiwa ni kuonesha kwa vitendo jinsi inavyowajali
wananchi hao.
Amesema wilaya zote mkoani Kagera zitaunganishwa na gridi
kwani kwa sasa no wilaya tatu tu ndio
zimeunganishwa na Gridi ya Taifa.
Ameahidi kuwa, Wananchi katika mkoa huo watakuwa watumiaji
wazuri wa umeme na walipaji bili wazuri iili TANESCO iendelee kupata mapato ya
kutekeleza miradi mingine.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba
amesema Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa
mikoa minne ambayo haijaunganishwa kwenye gridi ya Taifa ikiwemo Rukwa, Lindi
na Mtwara.
Amesema tukio la leo
ni la kihistoria kwani kukamilika kusainiwa kwa mikataba hiyo kunafanya mikoa
yote iliyo nje ya gridi kuwa kwenye mpango wa kupelekewa umeme gridi hivyo kwa sasa hakuna mkoa ulio
nje ya gridi ambao hauna mradi wa kupelekewa umeme.
Amesema kwa sasa Mkoa wa Kagera unapata umeme wa megawati 40
kutoka nchini Uganda kupitia kituo cha Kyaka na megawati 7 kutoka mwekezaji
binafsi wa mradi wa Mirongo/ Kikagati.
Amesema wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani
jumla ya mikoa sita kati ya 26 haikuwa imeunganishwa kwenye gridi ya Taifa ila
kwa kipindi cha minne Serikali imefanikiwa kuunganisha umeme Kigoma na Katavi
huku mingine iiliyosalia ikiwa miaradi inayoendelea kutekekelezwa.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (
TANZANIA), Lazaro Twange mradi huo una
umuhimu mkubwa mkoani Kagera kwani wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba,
Bukoba Vijijini na Manispaa ya Bukoba kwa muda mrefu sasa zimekuwa zikiitumia umeme kutoka nchini Uganda
takribani megawati 40 kupitia kituo cha kupoza umeme cha Kyaka ambacho
kinapokea umeme kutoka Masaka, Uganda kupitia njia ya umeme ya msongo wa
kilovoti 132 kufuatia mkataba wa makubaliano baina ya Tanzania na Uganda.
Pia, kukamilika kwa mradi huo kutawezesha kuunganishwa kwa kituo
cha kuzalisha umeme cha Kakono katika Gridi ya Taifa.
Amesema gharama za mradi ni shilingi bilioni 262.5 na
utatekelezwa kwa muda wa miezi 24.
Amesema.Mradi huu unatekelezwa kwa fedha za Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa
maendeleo ambapo Mfuko wa Maendeleo wa Shirika la Wauzaji Mafuta Duniani
(OPEC) utachangia dola za Marekani
milioni 60, Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi utachangia dola za Marekani milioni
30, Mfuko wa Maendeleo wa Saudia utachangia dola za Marekani milioni 13 na Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itachangia dola za Marekani milioni 2.6 kwa
ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi.
Amesema Wakandarasi watakaotekeleza mradi huo ni kampuni ya M/s. TBEA Co. Ltd kutoka nchini China ambayo itahusika na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Benako, na Kampuni ya M/s. Transrail Lighting Limited kutoka India itahusika na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Benako hadi Kyaka.
0 Maoni