DC Bagamoyo atoa onyo kali kwa wanaotorosha mkaa kupitia bandari bubu

 

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, ametoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na utoroshaji wa mazao ya misitu, hususan mkaa kupitia bandari bubu, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukaidi agizo hilo.

Onyo hilo limekuja baada ya operesheni ya pamoja iliyofanywa na Ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Kanda Maalumu ya Saadani, kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, kufanikisha kukamatwa kwa majahazi mawili yaliyobeba zaidi ya magunia 100 ya mkaa katika eneo la Mto Shanga, Bagamoyo.

Doria hiyo, iliyofanyika usiku wa kuamkia Agosti 23, 2025, ililenga kudhibiti biashara haramu ya mazao ya misitu kupitia bandari zisizo rasmi maarufu kama bandari bubu. Hata hivyo, watuhumiwa walitoroka na kutelekeza majahazi pamoja na mzigo wa mkaa uliokuwa umepakiwa.

Kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002 na miongozo yake, usafirishaji wa mazao ya misitu unapaswa kufanywa kupitia bandari rasmi pekee, ikiwemo Bandari ya Bagamoyo.

“Doria hizi ni endelevu na zinaendelea kufanyika katika maeneo yote ya bandari zisizo rasmi ili kuimarisha uhifadhi na kuzuia upotevu wa mapato ya serikali,” alisema DC Ndemanga.

Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo imetoa shukrani kwa Ofisi ya Muhifadhi Misitu Wilaya ya Bagamoyo, Hifadhi ya Taifa Saadani (SANAPA), Jeshi la Polisi na wadau wengine wa uhifadhi kwa ushirikiano katika utekelezaji wa jukumu la kulinda rasilimali za taifa.



Chapisha Maoni

0 Maoni