Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi.
Pili Mnyema, amefanya ziara ya siku moja
ya kikazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, yenye lengo la ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika
Halmashauri na kusikiliza na kutatua Kero za watumishi.
Akiwa katika ziara hiyo aliyoifanya
hapo jana, Bi. Mnyema amekutana na kufanya kikao kazi na watumishi wa Manispaa
ya Kibaha ambapo amesisitiza umuhimu wa ubunifu katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo kwa kusimamia vizuri na kuongeza mapato ya Halmashauri.
"Naomba tumuunge mkono Mheshimiwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kubuni
vyanzo vipya vya mapato. Hili ni moja ya maagizo niliyopatiwa na Serikali Kuu
ili kusaidia kuinua uchumi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha ," amesema
Bi. Mnyema.
Aidha, Katibu Tawala huyo amempongeza
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa ubunifu na
usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ambayo umechangia kuongezeka kwa mapato
ya Manispaa hiyo mwaka hadi mwaka.
Katika hotuba yake kwa watumishi,
amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kuwa na
nidhamu, uadilifu, uwajibikaji na bidii katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Pia amekemea matumizi mabaya ya fedha za umma na kusisitiza uaminifu katika
usimamizi wa rasilimali.
Katika ukaguzi wa miradi Bi. Mnyema
ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Shule
ya Awali na Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kata ya
Sofu, pamoja na mradi wa maduka ya biashara ya Kibaha Shopping Mall.
0 Maoni