Dkt. Nchimbi aahidi maji safi na barabara za lami Kwimba

 

Mgombea mwenza wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema chama hicho kimedhamiria kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wanapata huduma ya maji safi na salama.

Dkt. Nchimbi ametoa kauli hiyo jana katika mkutano wake wa kwanza wa kampeni, uliofanyika kwenye viwanja vya CCM Ngudu Wilayani Kwimba na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi wa wilaya hiyo na wamaeneo ya jirani.

“Tumedhamiria kuhakikisha wananchi wa Kwimba wanapata maji safi na salama, katika miaka hii mitano kila katika wanaKwimba 100, wanaKwimba 90 wapate maji safi na salama...asilimia 90 ya wanaKwimba wapate maji safi na salama,” alisema Dkt. Nchimbi.

Ameeleza kuwa wananchi wanajua CCM inavyotekeleza ahadi zake nyingi, hivyo asije akajitokeza mtu akahoji pale itakapotekeleza ahadi hiyo kwa kupitiliza na kufikia asilimia 95 ya wananchi hao kupata maji safi na salama.

Pia, amesema kuwa katika Ilani ya uchaguzi ya CCM kilio cha wananchi wa Wilaya ya Kwimba kupata barabara za lami kimesikika, “Rais Samia alituma watafiti wa CCM kuwauliza wananchi wanapenda nini ili waingize kwenye Ilani na wanaKwimba mlisema mnataka barabara za lami.”

Amesema katika kutekeleza hilo CCM kwa sasa imezidisha ujenzi wa barabara za lami kwa zaidi ya mara 30, ili kuhakikisha zinajengwa kilometa 120 za barabara za lami wilaya ya Kwimba kutoka kilomita 6 zilizojengwa miaka iliyopita. Pia, amesema watajenga na kuboresha barabara za changarawe.



Chapisha Maoni

0 Maoni