Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo amezindua Mpango wa Uwezeshaji wa Kiuchumi
kwa Vijana (YEE) ambao unagusa maeneo yanayopitiwa na mradi wa Bomba la Mafuta
Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ikiwa ni jitihada zinazoendelea kufanywa na
Serikali katika kuhakikisha kuwa jamii zilizo karibu na miradi zinanufaika na
miradi hiyo.
Akizindua mradi huo katika Kijiji cha
Bukombe, wilayani Bukombe, Mkoa wa Geita tarehe 18 Agosti 2025, Dkt. Biteko
amesema mradi huo wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi ni moja ya miradi iliyopangwa
kuwezeshwa na Kampuni ya EACOP kwa kipindi cha ujenzi na baada ya ujenzi ikiwa
ni sehemu ya Uwajibikaji wa Kampuni hiyo kwa jamii.
Amesema mradi huo umepangwa kuwafikia
zaidi ya vijana 12,261 ambapo miongoni mwao wanawake ni 6,130; wanaume 4,905 na
makundi maalumu ni 1,226 katika awamu ya kwanza inayohusisha Mikoa ya Geita,
Kagera, Tabora na Tanga.
" Tunapozindua mradi huu hatuna
budi kuwashukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa
Jamhuri ya Uganda. Viongozi wetu hawa kwa nia yao ya dhati na moyo wa uzalendo wameuendeleza na
kuusimamia kikamilifu mradi huu wa EACOP ambao umefikia asilimia 65, tumefikia
hapa sababu ya msukumo wao wa kutekeleza mradi huu" Amesema Dkt. Biteko.
Ameeleza kuwa tangu kuanza kwa mradi
wa EACOP mwaka 2022 hadi sasa, jumla ya Watanzania 9,194 wamepata nafasi za
kufanya kazi ndani ya mradi na hivyo kuwa fursa kwao ya kujipatia kipato, mwaka
2024 kampuni ilitoa mafunzo maalumu kwa Vijana 170 na kuwapatia kazi kwenye
mradi, Vijana wengine 110 wapo katika masomo na wanatarajiwa kujumlishwa pia
katika Mradi huo pamoja na kutoa ufadhili wa Vijana 238 katika vyuo mbalimbali
nchini.
Amesema wananchi wanaopitiwa na miradi
wanayo haki ya kunufaika na miradi lakini wana wajibu wa kulinda miundombinu ya
mradi na kuufanya kuwa ni sehemu yao kwani unachangia pia kubadilisha maisha ya
wananchi.
Pia, Dkt. Biteko ameipongeza kampuni ya
EACOP na Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) kwa kusimamia kwa ufanisi mradi huo huku akisisitiza kuwa, ili
wananchi waone mradi huo ni sehemu yao lazima waone faida zake hivyo miradi kama ya YEE inawapa chachu
wananchi kulinda miundombinu ya EACOP kwa
wivu mkubwa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko
amesisitiza kuwa, kampuni mbalimbali zinazotekeleza miradi kuhakikisha kuwa
hawaweki mkazo kwenye kuongeza ujuzi tu
kwa wananchi bali wanawapatia mitaji ili waweze kufanya vizuri zaidi.
Aidha, amewaasa vijana kuchangamkia
fursa zinazotokea kwenye miradi, wajitume, wawe waaminifu pale wanapopata fursa
na kueleza kuwa Serikali itaendelea kuwatengenezea fursa ili wajikwamue kiuchumi na kuleta maendeleo
nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya
Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Mhe. Patrobas Katambi amesema Rais, Dkt.
Samia Suluhu Hassan ametengeneza mipango mikakati ya kuhakikisha vijana
wanapewa fursa za ajira na mitaji kwenye maeneo mbalimbali ambapo mpango wa YEE
ni kielelezo cha matokeo ya mipango hiyo.
Ameeleza kuwa, kumekuwa na programu
mbalimbali ikiwemo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambapo kupitia programu hiyo
zaidi ya shilingi trilioni tatu zilitolewa kwa Watanzania takriban milioni 24 ikiwemo Wanawake, Vijana
na Makundi maalum kwa lengo la kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Mkuu wa Mkoa Geita, Martine Shigella
akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa inayopitiwa na mradi wa EACOP amesema
kuwa mradi wa EACOP ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo wananchi wa Geita
wamenufaika nayo kwa namna mbalimbali ikiwemo ajira za moja kwa moja na muda na
mfupi pamoja na mnyororo wa thamani
kupitia biashara ya vyakula, mbogamboga, matunda n.k
Amesema Mpango wa uwezeshaji wa vijana
kiuchumi ni matunda ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea
kuhakikisha vijana wanapata elimu na ujuzi hivyo mpango wa YEE unaongeza chachu
hiyo ya utoaji elimu na ujuzi kwa wananchi wakiwemo vijana.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,
Mhandisi Felchesmi Mramba amesema utekelezaji wa mradi wa EACOP wenye urefu wa
km 1443 ni moja ya miradi 17 inayotekelezwa na Wizara ya Nishati ikiwemo mradi
wa Julius Nyerere ( MW 2,115) ambao umekamilika, miradi ya umeme ya Ruhudji,
Rumakali na Malagarasi pamoja miradi mingine ya utafutaji na uzalishaji wa
mafuta na gesi asilia ukiwemo wa Eyasi Wembere.
Katika mradi wa EACOP amesema Serikali
imechangia shilingi trilioni 1.12 ambazo ni hisa za Tanzania na kuna kampuni za
kitanzania 200 ambazo zinafanya kazi mbalimbali katika mradi ambazo zitalipwa
jumla ya shilingi trilioni 1.325 ikiwa ni moja ya matunda ya uwepo wa mradi huo
nchini.
Akieleza sababu za kufanyika.kwa
uzinduzi wa mradi wa YEE wiiayani Bukombe amesema kuwa Bukombe kuna
kituo kikubwa zaidi cha kusukuma mafuta yatakayotoka nchini Uganda hadi
Chongoleani Tanga, kuna kambi kubwa ya mradi wa EACOP na pia kilometa 20 za
bomba hilo la mafuta zinapita katika eneo la Bukombe.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika
la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Makame ameeleza kuwa, TPDC
imeendelea kushirikiana na kampuni ya EACOP kuhakikisha kuwa mahitaji ya
wananchi yanabainishwa na kuzingatiwa katika utekelezaji wa mpango wa
Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Ameeleza kuwa mahitaji yaliyoainishwa
katika mradi wa YEE yaliandaliwa kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa kwa
ngazi ya vijiji, Kata na Halmashauri zilizopo maeneo linapopita bomba la
mafuta.
Awali Clare Haule - Meneja wa
Uwekezaji na Uwajibikaji kwa Jamii katika kampuni ya EACOP alisema mradi wa YEE
umeanzishwa kwa kutambua kwamba zaidi ya asilimia 65 ya idadi ya watu wa
Tanzania ni vijana chini ya umri wa miaka 35. Hata hivyo, vijana wengi hasa
katika maeneo ya vijijini wanakumbana na vikwazo vingi kama vile ukosefu wa
ajira, ukosefu wa mafunzo ya ufundi stadi , na ugumu wa kupata mitaji ya
kuanzisha au kukuza biashara.
Alisema awamu ya kwanza ya Mradi wa
YEE utawawezesha kiuchumi vijana katika
mikoa ya Geita, Kgera, Tabora na Tanga pamoja na mikoa mingine inayobaki
itanufaika katika awamu ya pili ambayo ni Singida, Shinyanga, Dodoma na Manyara
ambapo vijana watapewa ujuzi unaolingana
na mahitaji ya soko, kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha, na kuondoa
vikwazo vya ujasiriamali na ajira binafsi.
Aliongeza kuwa, Mradi wa YEE ni sehemu
ya Sera ya Uendelevu ya EACOP, chini ya nguzo ya Vizazi Vijavyo, inayolenga
kujenga uwezo wa vijana na kuongeza upatikanaji wa fursa za kiuchumi katika
jamii zinazoguswa na mradi.
0 Maoni