Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi
kuimarisha zaidi huduma za kijamii katika Jimbo la Chamwino, ikiwa ni pamoja na
sekta ya afya, upatikanaji wa maji safi na uboreshaji wa miundombinu ya
barabara.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Agosti 31,
2025, Chamwino mkoani Dodoma, Dkt. Samia amesema serikali ya CCM inaendelea na
jitihada za kuhakikisha wananchi wa jimbo hilo ambalo pia linahifadhi Ikulu ya
Rais wanapata huduma za msingi kwa ufanisi na kwa ukaribu zaidi.
“Niwaahidi kuwa tutakuja kuongeza vituo vya afya, vituo vya
afya 10 na zahanati nyingine tano. Jimbo la Rais halitakiwi kuwa na shida
yoyote ile, kwahiyo tutakuja kuongeza,” alisema Dkt. Samia huku akishangiliwa
na wakazi wa Chamwino waliohudhuria mkutano huo.
Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa maji, Dkt. Samia alisema
serikali imedhamiria kumaliza kabisa tatizo hilo. “Ninajua tuna shida ya maji,
mgombea ubunge hapa amesema mradi mkubwa upo, ninataka niwahakikishie
tutahakikisha Chamwino yote inapata maji kwa karibu zaidi,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo alieleza kuwa serikali
itatekeleza ujenzi wa barabara za lami kwa urefu wa kilomita 10 katika jimbo
hilo, sambamba na kuboresha barabara za changarawe ili kufungua fursa zaidi za
kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Chamwino.
Dkt. Samia alihitimisha kwa kuwataka wananchi wa Chamwino kuendelea kuiamini CCM na kumpa ridhaa ya kuongoza kwa awamu nyingine, akisisitiza kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji mshikamano, amani na uongozi thabiti.
0 Maoni