Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Florian Kabaka ameishukuru Serikali kwa
kuwezesha Wakala huo kutekeleza ujenzi wa daraja la Mohoro lenye urefu wa Mita
100 wilayani Rufiji.
Mhandisi Kabaka ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea
ujenzi wa daraja hilo pamoja na ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa Km. 4
zinazojengwa katika mji wa Ikwiriri wilayani humo.
“Niipongeze serikali kwa uwezeshaji huu kwa TARURA, kwakweli
uwepo wake hata wananchi wanaishukuru kwa kufungua miundombinu kila mahali,
nitoe heko kwa serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa TARURA pia nitoe heko kwa
menejimenti ya TARURA kwa usimamizi”.
Aidha, amewataka wananchi wa eneo hilo kulitunza daraja hilo
pamoja na vifaa vyote vinavyozunguka, pia kutochezea tuta la daraja hilo kwani
linaenda kuleta uhakika wa mawasiliano yao kwa mwaka mzima hususan kipindi cha
mvua.
“Daraja hili linaenda kuwaondolea shida iliyodumu kwa miaka
mingi lakini kuwafungulia fursa ya kujenga uchumi wao na Taifa kwa
ujumla".
Ameongeza kusema kuwa TARURA inaendelea kuondoa vikwazo vya
usafiri na usafirishaji kwa kuongeza mtandao wa barabara ili wananchi waendelee
kupata huduma na kufanya kazi za kuinua uchumi wa watanzania.
Naye, Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani, Mhandisi Leopold Runji
amesema kuwa mradi huo unaenda kuwasaidia wananchi kwani shughuli nyingi za
ukanda huo ni uchumi wa blue pamoja na kilimo cha mazao mchanganyiko hivyo
kukamilika kwa daraja hilo kutaondoa vikwazo kwa wakazi wa Mohoro.
Wakati huo huo Mhandisi Mkazi wa mradi huo, Emmanuel Mahimbo
amesema ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 48 ambapo wameshakamilisha ujenzi wa boksi
kalavati mbili, nguzo nne na sasa wanaongeza nguzo nyingine.
Ameongeza kuwa mpango kazi wao wa sasa hadi kufikia mwezi Januari 2016 wawe wamekamilisha sehemu ya daraja ili wabaki na kazi ya kukamilisha barabara hivyo ili kwenda na kasi hiyo, Mkandarasi ameanza kuingiza mashine na kuongeza watumishi ili kwenda na wakati.
0 Maoni