Jaji maarufu wa Marekani na nyota wa mitandao ya kijamii,
Frank Caprio, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88, familia yake
imethibitisha.
Katika taaluma yake ya zaidi ya miaka 40 huko Rhode Island,
alijulikana sana kwa kutumia huruma na ucheshi kutoa maamuzi yaliyotilia
maanani hali binafsi za watu waliokuwa mahakamani.
Video za Jaji Caprio akihukumu kesi katika kipindi chake
maarufu cha televisheni Caught in Providence zimeangaliwa na watu mabilioni
kwenye mitandao ya kijamii, na kumpatia umaarufu kama "hakimu mwema zaidi
duniani".
Kifo chake, kilichotokea baada ya kugunduliwa kuwa na
saratani ya kongosho, kilitangazwa kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram,
ambako atakumbukwa kwa "upole wake" na "imani yake isiyoyumba
juu ya wema wa watu".
Jaji Caprio alihudumu katika maelfu ya kesi katika mji wake
wa Providence, Rhode Island, kabla ya kuanza taaluma ya runinga.
Mtindo wake wa kipekee wa uendeshaji wa kesi ulisababisha vipande vya video kusambaa kwa kasi, ikiwa ni pamoja na kumwalika mtoto wa mtuhumiwa kukaa naye nyuma ya meza ya Jaji wakati wa kesi, kusema Jaji mdogo atanisaidia kutoa hukumu.
0 Maoni