Waziri wa Mambo ya
Nje wa Cyprus, Dkt. Constantinos Kombos, atatembelea Tanzania kuanzia tarehe 8
hadi 10 Julai kwa niaba ya Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya (EU) wa Mambo ya
Nje na Usalama / Makamu wa Rais wa Tume ya Ulaya, Kaja Kallas, katika jitihada
za kuimarisha ushirikiano kati ya EU na Tanzania na kushiriki katika mazungumzo
ya ngazi ya juu kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa.
Wakati wa ziara hiyo,
Waziri Dkt. Constantinos Kombos atakutana na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na
wawakilishi wa asasi za kiraia, viongozi wa biashara na wadau wengine kujadili
uhusiano wa EU na Tanzania, uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ushirikiano wa
kiuchumi chini ya mkakati wa Global Gateway, na maendeleo ya usalama katika
eneo la Maziwa Makuu.
Akizungumza kabla ya
ziara, Waziri Dkt. Constantinos Kombos alisema:
“Tanzania ni mshirika
wa kuaminika na thabiti katika eneo lenye umuhimu mkubwa. Tunaposherehekea
miaka 50 ya uhusiano kati ya EU na Tanzania mwaka huu, EU imejizatiti
kuimarisha ushirikiano wetu – kuanzia uwekezaji katika malighafi muhimu na
mabadiliko ya kidijitali hadi kuendeleza maadili ya kidemokrasia na ukuaji wa
pamoja. Pamoja tunaweza kufungua fursa mpya zitakazowanufaisha wananchi wa
Tanzania na washirika wa Ulaya.”
Balozi wa Umoja wa
Ulaya nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Christine Grau,
alisisitiza umuhimu wa ziara hiyo:
“Ziara hii inaakisi
dhamira ya EU ya ushirikiano imara na wa kimkakati na Tanzania, unaojengwa kwa
maslahi ya pande zote. Kufuatia ziara ya Waziri Kombo katika Makao Makuu ya EU
mwezi Aprili, hii ni ishara ya kuendelea kwa mazungumzo endelevu kati ya Umoja
wa Ulaya na Tanzania.”
Katika ziara hii,
masuala ya siasa yanayohusiana na pande zote, maendeleo ya kikanda, na
ushirikiano wa kiuchumi yatajadiliwa.
Hii ziara inafuatia
mikutano ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mheshimiwa Mahmoud Thabit
Kombo, iliyofanyika Brussels mwezi Aprili 2025 na Mwakilishi Mkuu wa EU wa
Mambo ya Nje na Usalama Kaja Kallas, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa
Kimataifa Koen Doens, na Makamu wa Rais wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya )EIB)
Thomas Östros, lengo la Mkutano huu
ilikuwa ni kuendeleza mazungumzo ya kisiasa, uwekezaji, na maendeleo endelevu.
0 Maoni