Matangazo ya moja kwa
moja kutokea hifadhi ya Ngorongoro yanayorushwa katika Banda la Wizara ya
Maliasili na Utalii ndani ya viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es Salaam yamekuwa
kivutio kikubwa kwa watembeleaji wa maonesho hayo.
Viongozi mbalimbali
wa Wizara ya Maliasili na Utalii akiwemo Naibu waziri wa Maliasili na Utalii
Mh.Dunstan Kitandula, Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi, Mkurugenzi wa Utalii Dkt.
Thereza Mugobi na viongozi wengine wamejionea matangazo hayo katika banda hilo.
Katika maonesho hayo
wananchi wamekuwa wakijionea vivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo Wanyamapori
vilivyopo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kupitia matangazo ya moja kwa moja
ambapo "Tv Screen" kubwa imewekwa katika banda hilo kuwezesha
wananchi kufuatilia.
Akizungumzia kuhusu
urushaji wa matangazo ya vivutio vya
utalii kutoka Ngorongoro mpaka sabasaba Afisa Uhusiano Mkuu wa Mamlaka ya
Hifadhi Ngorongoro Walter Mairo amesema ndani ya Banda la Wizara ya Maliasili
na utalii watembeleaji hupata fursa ya kuona jinsi wanavyoweza kutumia
teknolojia kuona vivutio wakiwa nyumbani.
“Hata baada ya
sabasaba unaweza kufuatilia matangazo yetu nyumbani kupitia kurasa zetu za
mitandaoni na kuona mubashara vivutio vyetu, kama unavyoona hapa spishi za
Wanyamapori mbalimbali na wageni walioko hifadhi tunawaona moja kwa moja tukiwa
hapa sabasaba,”alisema Mairo.
Maonesho ya 49 ya
sabasaba yanaendelea katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam ambapo
Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii limekuwa kivutio kikubwa.
Na. Hamis Dambaya -
DSM
0 Maoni