Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene
amewaonya wale wote wanaohamasisha uvunjifu wa amani nchini huku akiwasihi
Wanawake wasijiingize kwenye mtego huo
kwani madhara yake ni makubwa.
Mhe. Simbachawene ametoa
kauli hiyo leo wakati akifungua Kongamano la 16 la Wanawake Waombolezao Kitaifa
waliokusanyika jijini Dodoma kwa ajili ya kuombea amani ya nchi ya Tanzania hususan katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi
Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba
mwaka huu.
Amesema maendeleo
yaliyopo nchini ikiwemo huduma za kijamii ni matokeo ya amani na utulivu
uliopo, "Hatuwezi kubomoa ili tujenge upya, ni lazima tukumbatie
majadiliano kama Taifa hatuwezi tukawa tunafikiria sawa ni lazima tutofautiane,"
amesisitiza Mhe. Simbachawene.
"Kuna watu wanasema
Tanzania hii hakuna amani wala maendeleo
yaliyofanyika tangu tupate uhuru, hivyo tuandamane, hapo ndipo tutapata haki yetu, wananchi
kataeni huo ushetani," amesema
Waziri Simbachawene.
Kufuatia hatua hiyo Mhe. Simbachawene
amewataka Watanzania kuwapuuza wale wote
wenye maslahi binafsi wanaotaka kuwaona
wananchi wanachukiana wenyewe kwa wenyewe na hatimaye kuanza kuuana wao kwa wao kwa chuki za kupandikizwa.
Kwa upande wake, Askofu
Mkuu wa Tanzania Fellowship of Churches,
Godfrey Malasi amesema Kongamano hilo ni mahsusi kwa ajili ya maombi maalum ambayo yamekuwa yakifanyika
kila mwisho wa mwaka kwa lengo la
kuliombea amani Taifa la Tanzania na
kuwahimiza Watanzania kumjua na kumtumikia Mungu.
Sisi tunavyofurahia amani na utulivu
tuliyonayo, wenzetu huko kwingine wanalia na kusaga meno, hivyo tuna wajibu wa
kuzidi kumuomba Mungu atupe hekima ili tuzidi kuilinda amani yetu, amesisitiza
Askofu Malasi.
Vita sio nzuri
kabisa, sisi tumepewa uwezo wa kupigana
vita vya rohoni ili kuzuia vita vinavyoonekana, amesema.
Aidha, Askofu Malasi
amesema Kongamano hilo limekuwa likiombea maadili mema ya Taifa hususan katika
kipindi hiki ambacho vijana wameathiriwa na vitendo vya ushoga, usagaji na
utoaji mimba, vitendo ambavyo vinakwenda
kinyume na tamaduni zetu.
0 Maoni