WAZIRI MKUU Mhe. Kassim
Majaliwa amekutana na mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Grenada, Dickon Thomas
Mitchell na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza mahusiano kidiplomasia na
kibiashara kwa manufaa ya pande zote mbili.
Amesema kuwa Tanzania
itaendelea kutumia Jukwaa la Nne la Kibiashara na Uwekezaji kati ya Afrika na
Karibiani (ACTIF2025) kama daraja la kukuza ushirikiano katika maeneo ya
kipaumbele yakiwemo kilimo, uvuvi, afya na elimu ili kuwanufaisha wananchi wa
pande zote mbili.
Katika mazungumzo
yaliyofanyika ofisini kwa mwenyeji wake jijini St. George’s, Grenada, Waziri
Mkuu Majaliwa alisisitiza kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Grenada na
kubadilishana uzoefu katika teknolojia na maarifa ya kitaalamu hususan katika
sekta za uzalishaji na huduma ili kuimarisha uchumi wa viwanda na kuongeza
ajira kwa vijana.
Kwa upande wake, Mhe.
Mitchell alisema kuwa malengo ya nchi hiyo kupitia jukwaa la ACTIF ni kuhakikisha
kuwa nchi za Karibiani na Afrika, zikiwemo Tanzania na Grenada, zinajenga
misingi imara ya kiuchumi kwa kukuza biashara ya pande mbili katika maeneo
mbalimbali.
Viongozi hao
walikubaliana kuendelea kuhimiza majadiliano ya kiserikali baina ya nchi hizo
mbili na kushirikiana kwa karibu kufanikisha mikakati ya pamoja ya maendeleo,
huku wakisisitiza umuhimu wa mshikamano baina ya watu wa Afrika na Karibiani
kama msingi wa ustawi wa kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Waziri Mkuu
ameambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa SMZ,
Bw. Shariff Ali Sharriff na Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Karibe,
Marekani ya Kati na nchi za Venezuela na Guyana, Bw. Wilbroad Kayombo.
0 Maoni