Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) kwa mafanikio ya kutengeneza Mfumo Mkuu Jumuishi wa Kibenki (iCBS) kwa
kutumia wataalamu wa ndani, hatua iliyookoa zaidi ya Sh81 bilioni ambazo
zingetumika kununua mfumo kama huo kutoka nje ya nchi.
Dk. Mpango alitoa pongezi
hizo leo Julai 30, 2025, katika uzinduzi rasmi wa mfumo huo uliofanyika katika
Ofisi za BoT zilizoko Posta, jijini Dar es Salaam. Alisema mfumo huo una
viwango vya kimataifa na BoT imeweka historia kwa kuwa taasisi ya kwanza Barani
Afrika kutengeneza mfumo kama huo ndani kwa ndani.
“Kwa kutumia wataalamu wa
ndani, tumeokoa Sh81.32 bilioni. Huu ni ushahidi wa uwezo mkubwa tulionao kama
taifa,” alisema Dk. Mpango huku akisisitiza kuwa mfumo huo utaongeza ufanisi wa
benki hiyo katika kusimamia miamala ya kifedha bila vikwazo.
Makamu wa Rais aliitaka
BoT kushirikiana na taasisi kama TCRA, e-GA pamoja na wizara husika kuhakikisha
mfumo wa iCBS na mifumo mingine ya malipo inasimamiwa kwa weledi ili kuchochea
maendeleo ya kiuchumi.
Alihimiza matumizi ya
mifumo ya kidijitali katika miamala badala ya kutegemea fedha taslimu, akisema
ni njia ya kisasa ya kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza uwazi
katika sekta ya fedha.
Katika hatua nyingine,
Dk. Mpango alitoa agizo kwa BoT kuchukua hatua kali dhidi ya wakopeshaji wa
mitandaoni ambao wamekuwa wakiwabana wananchi kwa riba kubwa na ukiukaji wa
faragha kwa kusambaza taarifa zao bila idhini.
“Wakopeshaji hawa siyo tu
wanatoza riba kubwa, bali wanadhalilisha wananchi. BoT ichukue hatua haraka na
iendelee kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mikopo salama na halali kutoka benki
zilizosajiliwa,” alisema.
Makamu wa Rais pia
alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mfumo wa iCBS unalindwa kisheria kupitia
mifumo ya hakimiliki, huku akizitaka wizara husika kutoa motisha kwa wabunifu
wa ndani wanaoleta suluhisho bunifu kwa changamoto za kitaifa.
Amesema Serikali
itaendelea kuboresha mazingira ya ubunifu na utafiti nchini kwa kuongeza bajeti
ya utafiti, kuanzisha vituo vya ubunifu na kuongeza ushirikiano kati ya sekta
binafsi na taasisi za elimu ya juu.
Kwa upande wake, Gavana
wa BoT, Emmanuel Tutuba alisema mfumo wa iCBS umeleta maboresho makubwa katika
utoaji wa taarifa za serikali, usimamizi wa miamala ya kifedha, ukokotoaji wa
riba na uandaaji wa taarifa kwa wahisani na wadau wengine wa maendeleo.
Alisema hali ya uchumi
nchini imeendelea kuimarika ambapo thamani ya Shilingi ya Tanzania imekuwa
thabiti na mfumuko wa bei kudhibitiwa. Kufikia Juni 2025, akiba ya fedha za
kigeni imefikia dola bilioni 6.2 , kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa.
Kuhusu ununuzi wa
dhahabu, Tutuba alisema baada ya marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2024,
BoT imeweza kununua tani 6.6 za dhahabu safi zenye thamani ya dola milioni
706.6, sawa na asilimia 110 ya lengo la mwaka.
Katika hafla hiyo, Dk.
Mpango pia alifunga rasmi Makumbusho ya Benki Kuu ya Tanzania ambayo itaonesha
historia ya benki hiyo. Aidha, alizindua rasmi Maktaba ya Mtandao ya BoT,
itakayowawezesha wananchi na watafiti kupata vitabu na majarida kwa njia ya mtandao.
0 Maoni