Saratani ya ini iko katika njia ya kuwa janga kubwa zaidi la kiafya duniani, hasa kwa watu wazima wa umri mdogo, huku visa vya ugonjwa huo vikitarajiwa kuongezeka maradufu kufikia mwaka 2050, wataalamu wameonya.
Awali saratani ya ini
ilionekana kuwa ugonjwa unaowakumba zaidi wazee waliokuwa na maambukizi ya homa
ya ini (hepatitis) au utegemezi wa pombe. Hata hivyo, kwa sasa ugonjwa huu
unazidi kugundulika kwa watu wenye umri wa miaka 30 na 40.
Uchambuzi mkubwa mpya
uliochapishwa kwenye jarida la The Lancet umehusisha mabadiliko haya na
kuongezeka kwa unene wa kupindukia (obesity) pamoja na magonjwa yanayohusiana
na ini kama vile MASLD (ugonjwa wa ini unaohusiana na hitilafu ya kimetaboliki
na mafuta kwenye ini).
Ripoti hiyo inakadiria
kuwa idadi ya visa vipya vya saratani ya ini duniani itaongezeka kutoka visa
870,000 mnamo 2022 hadi kufikia milioni 1.52 ifikapo mwaka 2050. Vifo vya kila
mwaka kutokana na ugonjwa huo vinatarajiwa kuongezeka kutoka 760,000 hadi
milioni 1.37 katika kipindi hicho.
Wataalamu wanasema kwamba
mojawapo ya visababishi vinavyoongezeka kwa kasi ni MASH (aina kali ya MASLD),
hali mbaya ya ugonjwa wa ini yenye mafuta inayohusishwa na unene wa kupindukia
na matatizo ya kimetaboliki.
Idadi ya saratani ya ini
inayosababishwa na MASH inatarajiwa kuongezeka zaidi ya mara mbili – kutoka
asilimia 5 mwaka 2022 hadi asilimia 11 mwaka 2050.
Wakati huohuo, idadi ya
visa vinavyosababishwa na virusi vya hepatitis B – ambavyo kwa sasa ndiyo
chanzo kikuu cha saratani ya ini – inatarajiwa kupungua. Vivyo hivyo, visa
vinavyosababishwa na virusi vya hepatitis C navyo vinakadiriwa kupungua kwa
kiasi fulani.
Hata hivyo, idadi ya visa
vinavyotokana na unene wa kupindukia na unywaji pombe inatarajiwa kuongezeka
katika kipindi hicho hicho.
Kufikia mwaka 2050, zaidi
ya robo ya visa vya saratani ya ini vitasababishwa na pombe, na kimoja kati ya
kila visa kumi kitasababishwa na aina kali ya MASLD, ambayo zamani ilijulikana
kama ugonjwa wa ini lenye mafuta.
Hali hiyo hutokea pale
mafuta yanapokusanyika kwenye ini la mtu, na inahusishwa sana na unene wa
kupindukia na ugonjwa wa kisukari aina ya pili.
Timu ya watafiti kutoka
Hong Kong imebainisha kuwa asilimia 60 ya visa vya ugonjwa huu hatari vinaweza kuzuilika.
Kuhusu matokeo ya utafiti
huo, watafiti wamesema yanadhihirisha haja ya kuchukua hatua za kinga dhidi ya
saratani ya ini, inayojulikana pia kama hepatoselula kansa (hepatocellular
carcinoma).
Matibabu makuu ya MASLD
ni kula lishe bora, kuwa na shughuli za mwili mara kwa mara, na inapobidi
kupunguza uzito.
“Saratani ya ini ni
tatizo linalozidi kuwa kubwa kiafya duniani,” alisema Profesa Jian Zhou, Mwenyekiti
wa Kamisheni hiyo kutoka Chuo Kikuu cha Fudan, China.
0 Maoni