Taasisi na asasi za
kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu
wa mwaka huu zimetakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo
ya Tume.
Wito huo umetolewa na
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani, Jacobs
Mwambegele wakati akifungua mkutano wa Tume
na taasisi na asasi hizo leo
Julai 30, 2025 jijini Dar es Salaam.
”Nitoe rai kwenu haswa
wale mliopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kuzingatia sheria, kanuni na
maelekezo ya Tume wakati wote wa utekelezaji wa zoezi hilo la kutoa elimu ya
mpiga kura,” amesema Jaji Mwambegele.
Amesisitiza kuwa katika
kipindi cha uchaguzi Tume itafanya kazi kwa karibu na taasisi na asasi za
kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura.
”Niwaombe msichoke
kuwasisitiza na kuwahimiza wadau na wananchi kwa ujumla kuzingatia Sheria za
Uchaguzi, Kanuni na Maelekezo ya Tume. Tume nayo kwa upande wake itaendelea
kuzingatia Sheria za Uchaguzi na Kanuni katika michakato yote ya
uchaguzi,”amesema.
Jaji Mwambegele ameongeza
kuwa wakati wa kampeni uzoefu unaonesha kuwa kunakuwa na joto la kisiasa
linatokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu wa kisiasa, hivyo ameziasa
taasisi na asasi hizo kutumia nafasi yao kuwaelimisha wananchi ili uchaguzi
ufanyike kwa amani na utulivu.
”Kipindi hicho cha
kampeni mnapaswa kuwahimiza wananchi kupitia majukwaa yenu kuwa makini kwa
kuhakikisha kuwa hawawi chanzo cha kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu,”
amesema.
Kwa mujibu wa kifungu cha
10(1)(g)(h) na (i) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka
2024, Tume inao wajibu wa kutoa elimu ya mpiga kura nchini, kuratibu na kusimamia
taasisi na asasi zinazotoa elimu ya mpiga kura na kualika na kusajili
waangalizi wa uchaguzi.
Kwenye uchaguzi mkuu wa
mwaka huu Tume imetoa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura kwa taasisi na asasi 164 kwa ajili ya kutoa elimu
ya mpiga kura na taasisi na asasi 76 za
ndani na 12 za kimataifa zimepata kibali cha uangalizi wa uchaguzi.
Baadhi ya wawakilishi wa
taasisi na asasi hizo wamesema wamejipanga rasmi kutoa elimu ya mpiga kura
haswa kwa vijana wanaotarajia kupiga kura kwa mara ya kwanza.
Wamesisitiza kuwa watatoa
elimu kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo ya Tume.
Mwenyekiti wa Malezi
Foundation Network, Mwalimu Neema Kabale,
amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa vijana walioandikishwa kuwa
wapiga kura kwa mara ya kwanza wanapata uelewa wa kutosha kuhusu taratibu za kupiga kura.
0 Maoni