Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa Mradi wa
Uchimbaji na Uchakataji Madini ya Urani uliopo katika Eneo la Mto Mkuju, Wilaya
ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma, ni hatua ya kimkakati itakayoiweka Tanzania katika
ramani ya dunia kwa kuifanya kuwa miongoni mwa mataifa kumi yanayoongoza kwa
uzalishaji wa madini hayo muhimu duniani.
Amesema hayo leo Julai
30, 2025, wakati akizungumza na wananchi katika hafla ya uzinduzi rasmi wa
Kiwanda cha Majaribio cha kuchenjua madini ya urani kilichopo Mto Mkuju, hatua
inayoashiria mwanzo wa safari ya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na
uchakataji wa urani barani Afrika.
Rais Samia amesema kuwa,
hatua hiyo ni ssehemu ya mkakati wa Tanzania kufikia uchumi wa kati kupitia
matumizi bora ya rasilimali asilia, ikiwemo madini ya urani ambayo yana thamani
kubwa kimataifa.
“Ni siku ya historia kwa
nchi yetu, kwani Tanzania inaanza rasmi safari ya kuwa mzalishaji mkubwa wa
madini ya urani duniani kwa mara ya kwanza katika kiwango hiki. Urani ni moja
ya madini mkakati tuliyobarikiwa kuwa nayo, na upatikanaji wake utachangia
katika kuzalisha nishati salama na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika sekta
ya madini duniani,” amesema Rais Dkt. Samia.
Rais Dkt. Samia amesema
kuwa, kwa hatua hiyo, Tanzania inajiweka kuwa kitovu cha utafiti na uchakataji
wa urani duniani na Afrika, hatua itakayofungua fursa mpya za kiteknolojia,
kitaaluma na kiuwekezaji nchini na kuifanya Tanzania kuingia katika ramani ya
dunia kuwa miongoni mwa nchi 10 zinazozalisha urani duniani, na hivyo kuvutia
uwekezaji wa kimataifa katika sekta ya madini mkakati.
Ameongeza kuwa, Sekta ya
Madini ni miongoni mwa vipaumbele vya Dira ya Taifa ya 2050, kwq kwamba kupitia
sekta hiyo, Tanzania inalenga kukuza uchumi wa viwanda unaotumia teknolojia ya
hali ya juu pamoja na usimamizi bora wa rasilimali madini.
Manufaa ya Mradi huu ni
pamoja na Gawio la Serikali ambapo Asilimia 20 ya hisa zinazomilikiwa na
Serikali zinatarajiwa kuleta takribani dola milioni 40 kwa mwaka, fedha
zitakazosaidia miradi ya maendeleo. Manufaa mengine ni pamoja na ajira kwa
Watanzania, utafiti, mapato na mrabaha.
Aidha, Rais
Samia ameelekeza Mradi huo kuwa shirikishi kwa jamii kupitia miradi ya kijamii
(CSR) ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara sambamba na
kuzingatia taratibu za ulindaji mazingira ili kulinda mfumo wa ikolojia wa eneo
la Mto Mkuju.
Kwa upande wake,
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amemshukuru Rais Samia kwa kuipa sekta
ya madini kipaumbele, jambo lililopelekea kuanzishwa kwa miradi mikubwa ikiwemo
huo wa Mkuju.
Amesema mradi huo ni
mkubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati, na Tanzania sasa inakuwa miongoni mwa nchi
tano pekee barani Afrika zenye miradi mikubwa ya uzalishaji urani wa aina hiyo
na kwamba hatua hiyo ni matokeo ya mazingira rafiki kwa uwekezaji
yaliyoandaliwa na Serikali chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Waziri Mavunde amesisitiza
kuwa Sheria ya Madini inawataka wamiliki wa leseni kuhakikisha jamii
zinazozunguka miradi zinanufaika moja kwa moja kupitia miradi ya kijamii (CSR).
Naye, Rais wa Kampuni ya
Uranium One, Pavel Larionov, amesema kuwa mradi huo utakuwa ukizalisha
takribani tani 300,000 za urani kila mwaka, na unatarajiwa kuimarisha
upatikanaji wa madini hayo kimataifa huku Tanzania ikipata mapato na nafasi za
ajira kwa wingi.
0 Maoni