Serikali imewataka wakuu
wa taasisi za umma kutengeneza mazingira rafiki ya kazi yatakayowawezesha
watumishi kuongeza tija na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kauli hiyo ilitolewa na
Mhe. Ridhiwani Kikwete, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana na
Wenye Ulemavu, alipokuwa akifunga mafunzo elekezi ya siku nne kwa Watendaji
Wakuu wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali - Kundi la Pili,
Jumatano, Julai 30, 2025, katika Shule ya Uongozi ya Mwl. Julius Nyerere,
Kibaha, Pwani.
Katika hotuba yake,
Waziri Kikwete aliwataka wakuu wa taasisi za umma kusimamia vizuri
rasilimaliwatu ikiwa wanataka kuongeza ufanisi wa taasisi wanazoziongoza.
“Ikiwa mnataka kupata
matokeo mazuri, mnapaswa kuepuka kuwa miungu watu na badala yake tengenezeni
mazingira mazuri ambayo yatawahamasisha watumishi kujituma, kuleta ubunifu na
kuongeza tija katika kila ngazi ya utendaji,” alisema Mhe. Kikwete.
Mhe. Kikwete aliendelea
kwa kutoa angalizo, “Lakini simaanishi muwachekee wazembe. Ninachomaanisha ni
nyie kufanya kazi kwa msukumo, weledi na kuzingatia misingi ya utawala bora.”
Hii inamaanisha kuwa
wakuu wa taasisi wanapaswa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na
kuhakikisha kwamba kila mfanyakazi anahisi kuheshimiwa na kuwa na nafasi ya
kutoa mawazo ambayo yataboresha huduma na kuleta mabadiliko chanya.
Hii, alisema, ni njia ya
kuhakikisha taasisi zinakuwa na tija kwa muda mrefu na kuendana na mabadiliko
ya kiteknolojia na kiutendaji.
Mageuzi yanayoendelea
katika kuimarisha utendaji kazi na usimamizi wa Taasisi za Umma yameongeza
uwezo wa Serikali kufaidika na uwekezaji wa Sh86.29 trilioni.
Hili linadhihirishwa na
gawio la mwaka wa fedha 2024/25, ambapo Mhe. Rais. Dk. Samia Suluhu Hassan
alikabidhiwa Sh1.028 trilioni kama mapato yasiyo ya kikodi kutoka kwa taasisi,
Mashirika ya Umma, Wakala za Serikali na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa
hisa chache.
“Kiasi hicho ni cha
kihistoria. Lengo letu la msingi ni kuhakikisha kuwa uwekezaji wa Serikali
katika Taasisi na Mashirika ya Umma unaendelea kuleta tija kwa Taifa letu kwa
mfumo endelevu,” alisema Mhe. Kikwete.
Kwa upande wake Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo, alisema
kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina serikali itahakikisha inatengeneza mazingira
ambayo yatapelekea kutimia kwa maono ya Mhe. Rais ya kujenga Taasisi, Mashirika
ya Umma na Wakala za Serikali imara na zenye uwezo wa kuharakisha kufikiwa kwa
maendeleo ya Taifa letu.
Aidha, Prof Mkumbo
alisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa miongozo ya serikali na sheria zinazohusu
usimamizi wa taasisi, kwa lengo la kudhibiti matumizi yasiyo na tija na
kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma kwa manufaa ya taifa.
Katibu Mkuu, Ofisi ya
Rais (Utumishi), Bw. Juma Mkomi, alisema mafunzo kwa wakuu wa taasisi,
yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na Taasisi ya
Uongozi, ni kitendea kazi kikubwa kwani yamegusa rasilimali watu.
Mafunzo hayo yaliyowaleta
pamoja wakuu wa taasisi 114 yamewapa washiriki ujuzi na mbinu za kisasa za
usimamizi, ikiwemo kuendeleza utamaduni wa uwajibikaji, uwazi, na ufanisi
katika taasisi zao.
“Ni imani yangu mafunzo
yataongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali watu,” alisema Bw. Mkomi huku
akiongeza kuwa, “kujifunza ni suala endelevu, msione haya kujifunza kutoka kwa
wasaidizi wenu.”
“Ukijifunza kutoka kwao,
wataona na wao ni sehemu ya uendeshaji wa taasisi na hivyo watafanya kazi kwa
kujituma na ufanisi Zaidi.”
Kwa upande wake Msajili
wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema ili kufanikisha safari ya mageuzi ya
mashirika ya umma, inahitajika uongozi thabiti, ubunifu, na mshikamano wa pamoja
kati ya taasisi za umma, Wizara mama, Ofisi ya Msajili wa Hazina na wadau
wengine wa serikali.
Aliwahimiza watendaji
wakuu kuendelea kujifunza na kubadilisha mtazamo wao ili kuendana na mageuzi ya
utawala bora yanayohitajika kufanikisha maendeleo endelevu ya taifa.
“Tunaweza kuupata ufanisi
wa matokeo chanya kama uongozi utakuwa na ufanisi,” alisema huku akiongeza kuwa
Ofisi ya Msajili wa Hazina itaendelea kufanya mageuzi ili taasisi zilete tija
iliyokusudiwa.
0 Maoni