Hatua ya Donald Trump
ya kupunguza kwa kiasi kikubwa ufadhili wa Marekani kwa misaada ya kibinadamu inaweza
kusababisha vifo vya ziada zaidi ya milioni 14 kufikia mwaka 2030, kwa mujibu
wa utafiti uliochapishwa katika jarida la kitabibu la The Lancet.
Utafiti huo unaonesha
kuwa theluthi moja ya waliopo hatarini kufa mapema ni watoto.
Waziri wa Mambo ya
Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema mwezi Machi kuwa serikali ya Rais Trump
ilikuwa imefuta zaidi ya asilimia 80 ya mipango yote ya Shirika la Maendeleo la
Kimataifa la Marekani (USAID).
Kwa mujibu wa Davide
Rasella, mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo kutoka The Lancet, "Kwa nchi
nyingi za kipato cha chini na cha kati, mshtuko utakaotokana na hatua hii
utalingana na athari za janga la dunia au machafuko ya kivita."
Rasella, ambaye pia
ni mtafiti katika Taasisi ya Afya ya Kimataifa ya Barcelona, aliongeza kuwa
kupunguzwa kwa ufadhili huo "kunahatarisha kusitisha ghafla na kurudisha
nyuma mafanikio ya miongo miwili katika afya ya jamii zilizo hatarini."
Ripoti hii
inachapishwa wakati viongozi kadhaa wa dunia wanakutana katika jiji la Seville,
Hispania, kwa ajili ya mkutano wa misaada unaoongozwa na Umoja wa Mataifa,mkutano
mkubwa zaidi wa aina yake katika kipindi cha miaka kumi.
Kwa kuangalia data
kutoka nchi 133, timu ya watafiti ilikadiria kuwa ufadhili wa USAID ulisaidia
kuzuia vifo milioni 91 katika nchi zinazoendelea kati ya mwaka 2001 na 2021.
0 Maoni