Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof. Tumaini Nagu amewataka Maafisa Lishe kuimarisha elimu ya lishe kwa jamii ili kudhibiti udumavu na ukondefu kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 pamoja na uzito uliopitiliza kwa watu wazima.
Prof. Nagu ametoa
agizo hilo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa uratibu wa masuala ya lishe
nchini kwa maafisa lishe wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa waliokutana
Jijini Dodoma kwa muda wa siku mbili kujadili namna ya kufanya maboresho katika
utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Katika maelekezo yake
kwa watendaji hao, Prof. Nagu amesema Taifa linawategemea sana kubadilisha afya
za watanzania hasa kwa kutoa elimu zaidi na kuishauri jamii juu ya ulaji bora
ili kukabiliana na matatizo ya lishe.
“Nyie ndio jiwe la
msingi kuhakikisha kuwa takwimu mbovu za lishe tulizonazo zinabadilika, tufanye
kazi kweli ili tuwe na sababu ya kutembea kifua mbele kwamba tumeibadilisha
jamii, kwa kuhakikisha tunatoa elimu juu ya ulaji bora na tunatekeleza program
zinazowekwa kitaifa zenye lengo la kuboresha afya ya jamii yetu kupitia lishe
bora,” alisema Prof. Nagu.
Awali akisoma risala
ya maafisa lishe hao January Dalushi amewasilisha ombi kwa Serikali na
kuielekeza Taasisi ya MSD kuagiza Chakula Dawa ili vituo viweze kununua kwa
urahisi, huku wakiomba Maafisa Lishe wawe moja ya Wataalam wanaoajiriwa kwenye
Taasisi hiyo ili kutoa ushauri wa kitaalam kwenye bidhaa mbalimbali za Lishe
zinazonunuliwa na Bohari ya Dawa ya Taifa.
Ajenda ya lishe
inatajwa kuwa miongoni mwa vipaumbele muhimu vya kiuchumi ulimwenguni kote
kutokana na athari za matatizo ya lishe katika ukuzaji wa uchumi na kuleta
maendeleo endelevu ya ulimwengu ifikapo 2030.
Na. OR - TAMISEMI
0 Maoni