TFS yatoa elimu ya biashara ya mazao ya nyuki, wananchi waitwa kunufaika

 

Wananchi wamehimizwa kuchangamkia fursa ya kufanya biashara ya mazao ya nyuki kufuatia elimu iliyotolewa jana Julai 8, 2025 na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika banda lao lililopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii.

Akizungumza wakati akitoa elimu hiyo, Mhifadhi Mwandamizi wa TFS, Grace Buchukundi, alisema biashara ya mazao ya nyuki ni moja ya sekta zenye fursa kubwa lakini bado wananchi wengi hawana taarifa sahihi za kisheria na kiutendaji kuhusu namna ya kuingia sokoni.

“Sheria ya Ufugaji Nyuki Na.15 ya mwaka 2002 na Kanuni zake za mwaka 2005 zimeweka misingi ya usimamizi wa ubora na usalama wa mazao ya nyuki. Kila mfugaji au mfanyabiashara anatakiwa kusajiliwa katika Ofisi za TFS za Wilaya husika,” alisema Buchukundi.

Mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo, Mohamed Juma, alisema elimu hiyo imemfungua macho baada ya muda mrefu kutamani kuingia kwenye biashara ya mazao ya nyuki bila kufahamu hatua zinazohitajika.

“Nimepata kuelewa kuwa ili kuanza, lazima uwe na nyaraka muhimu kama leseni kutoka BRELA, kitambulisho cha Taifa (NIDA), hati ya mlipa kodi (TRA) na muhtasari wa kampuni kwa wale wenye kampuni. Pia kuna ada ya usajili ya Shilingi 53,000 kwa mwaka na gharama za ukaguzi wa ubora,” alisema.

Kwa mujibu wa Buchukundi, wafanyabiashara wa ndani na wale wanaokusudia kuuza asali na nta nje ya nchi wanatakiwa pia kulipia ada za vibali na usafi kulingana na uzito wa shehena. Ada za kuuza nje huanzia Shilingi 110,000 kwa mwaka mmoja wa kiserikali.

Akitoa wito kwa umma, TFS imewataka wananchi kufika katika banda lao kupata elimu zaidi pamoja na kununua Misitu Honey, asali safi na bora inayozalishwa na Wakala huo. Aidha, wananchi wanahimizwa kununua miche na mbegu bora za miti ili kuchangia uhifadhi wa misitu na ustawi wa mazingira.

“Tunakaribisha wananchi waje kujipatia asali yenye ubora na miche bora kwa bei nafuu. Lengo letu ni kuhakikisha jamii inanufaika na rasilimali za misitu kwa njia endelevu,” aliongeza Buchukundi.

Maonesho hayo yanatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa wiki hii huku wananchi wakihimizwa kuchangamkia fursa zilizopo.



Chapisha Maoni

0 Maoni