Hatimaye binti wa
Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, Diana Kamuntu, ametangaza rasmi kuwa
yuko single, baada ya ndoa yake ya miaka 18 kuvunjika kisheria.
Diana, ambaye
alizaliwa mwaka 1980, ni mtoto wa pili wa Rais Museveni na Mkewe Janet Kataaha
Museveni. Alifunga ndoa na mfanyabiashara Geoffrey Kamuntu tarehe 24 Julai
2004, ndoa ambayo ilijaliwa watoto watatu, wavulana wawili na msichana mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa
zilizothibitishwa, Mahakama ilitoa uamuzi wa kuvunjika kwa ndoa hiyo mnamo
mwaka 2022 kupitia amri ya kisheria ya Decree Nisi, ambayo huashiria hatua ya
awali ya talaka kabla ya kuwa rasmi (Decree Absolute).
Katika hatua ya hivi
karibuni, Diana ametangaza kuachana rasmi na jina la ukoo wa aliyekuwa mumewe,
“Kamuntu”, na kurejea kutumia jina la familia ya mzazi wake, sasa
akijitambulisha kama Diana Museveni Kyaremera.
Ingawa sababu za
kuvunjika kwa ndoa hiyo hazijawekwa wazi, vyanzo vya karibu vinaeleza kuwa
wawili hao walikuwa na tofauti zisizoweza kupatanishwa kwa muda mrefu.
Wakati familia ya
Museveni kwa kawaida huepuka kuweka maisha yao binafsi wazi kwa umma, hatua ya
Diana kutangaza hali yake ya ndoa imezua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya
kijamii, huku wengi wakitoa maoni mbalimbali kuhusu uamuzi huo.
Hadi sasa, upande wa
Geoffrey Kamuntu haujatoa kauli yoyote rasmi kuhusu suala hilo.
0 Maoni