WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya ufanyaji
biashara za huduma za kifedha ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje kwa kuwa
maendeleo endelevu ya taifa hayawezi kufikiwa bila ushiriki thabiti wa sekta
binafsi.
Amesema kuwa sekta ya
fedha ni kichocheo kikubwa katika ukuaji wa Uchumi na ustawi wa wananchi kwa
ujumla na ni moja ya sababu inyowezesha maendeleo ya Taifa kwenda kwa kasi.
Amesema hayo leo
Alhamisi (Julai 03, 2025) wakati wa uzinduzi wa Benki ya Maendeleo PLC, kuwa
Benki kamili ya kibiashara, kwenye ukumbi wa mikutano wa hotel ya Hyatt Regency
jijini Dar es Salaam.
“Endeleeni kuimarisha
ushirikiano miongoni mwenu, serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta ya fedha
katika kuchagiza maendeleo, imeendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia
bunifu.”
Katika hatua
nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa taasisi zote za kifedha zikiwemo
benki kuongeza juhudi katika kutoa elimu ya kifedha kwa wananchi ili kuwajengea
uwezo wa kuelewa, kutumia na kunufaika na huduma za kifedha kwa maendeleo yao
binafsi na kwa ustawi wa taifa kwa ujumla.
“Tukifanya haya
tutapunguza wizi, upotevu wa fedha kiholela kwa sababu kila mmoja atakuwa
anaweza kujua fedha yake ataipataje, ataihifadhi wapi na namna ya kutoa lakini
pia wapeni wateja wenu namna ya utunzaji wa fedha.”
Pia, Mheshimiwa
Majaliwa ameongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa Finscope huduma
jumuishi za fedha zimeweza kukua kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi kufikia
asilimia 76 mwaka 2023. “kwa mujibu wa utafiti huo, matumizi ya huduma za benki
yameongezeka na kufikia asilimia 22 mwaka 2023 kutoka asilimia 17 mwaka 2017.”
Kadhalika, Mheshimiwa
ametoa wito kwa taasisi zote za fedha zijenge mifumo rahisi na rafiki kwa
makundi yote ya watumiaji wa huduma za kifedha.
Awali, Akizungumza
kwa niaba ya Askofu Mkuu wa Kanisa la KKKT na Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na
Pwani Dkt. Alex Malasusa, Muwakilishi wa Askofu Dean Chadiel Lwiza ameishukuru
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kuisimamia benki hiyo na kuwa mfano wa benki iliyoanzishwa
na wazawa kwa mtaji mdogo hadi kufikia kuwa benki kitaifa. “Tunaiomba benki kuu
jicho lenu liwe kali kuliko letu, itazameni hii benki.”
Kadhalika, ameongeza
kuwa sera nzuri na mazingira mazuri ya uwekezaji katika biashara na usimamizi
mzuri za biashara. “Tunaishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoomgizwa na Rais
Dkt. Samia kwa kuendelea kuweka mazingira haya mazuri ya ufanyaji biashara.”
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa Maendeleo Bank PLC Lomnyaki Saitabau amesema kuwa benki hiyo
imejiweka katika nafasi bora zaidi ya kuwa benki ya kisasa, shindani na
jumuishi kwa Watanzania wote hasa kipindi dunia inapoelekea kwenye zama mpya
zenye msukumo wa kiteknolojia, ubunifu, na uwajibikaji wa hali ya juu.
“Kwa kufanya hivyo,
tunaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassani, yenye dhamira ya
kuwafikia watanzania wengi zaidi nchi nzima kupitia dira ya taifa ya
ujumuishaji wa kifedha (financial inclusion) na kuchochea maendeleo ya kiuchumi
kupitia sekta binafsi, tutaendelea kushirikiana na Serikali, katika ujenzi wa
Uchumi wa nchi.”
Naye, Naibu Waziri wa
Fedha Hamad Hassan Chande ameipongeza benki hiyo kwa hatua kuwa iliyofikiwa na
benki hiyo katika utoaji huduma kwa watanzania hasa kwa kutumia fursa
zilizowekwa na Serikali “Sisi Wizara ya Fedha tumeendelea kuweka mazingira
mazuri na rafiki ya ufanyaji wa shughuli za kifedha, sasa wekeni mkakati wa
kuifikisha benki hii maeneo mengi zaidi.”
0 Maoni