Muhimbili na Vodacom wafanikisha matibabu ya bure kwa watu 3,800 Tanga, Kilimanjaro

 

Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation imehitimisha kambi ya ya siku sita katika mikoa ya Tanga na Kilimanjaro kuanzia tarehe 21 hadi 27 Julai, 2025 ambapo katika kambi hiyo wananchi takribani 3,800 wamenufaika na huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi bure.

Katika kambi hiyo wananchi waliofanyiwa uchunguzi na matibabu ya macho ni 1,499 Magonjwa ya ndani 1,207, Afya ya kina mama na uzazi 867, Masikio, Pua na Koo 803, tathmini ya watu wenye ulemavu 813, huduma ya afya ya watoto 700, Afya ya Kinywa na Meno 671, Saratani 756, Ngozi 621 na afya ya akili 553.

Aidha kati ya wagonjwa 1,499 waliofanyiwa uchunguzi wa macho walibainika kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukavu wa macho, mzio, uoni hafifu, kushindwa kusoma maandishi madogo ya karibu, mtoto wa jicho na shinikizo la macho.

Akielezea sababu kubwa inayochangia watu kupata changamoto za macho katika maeneo hayo, Daktari Bingwa wa Macho, Dkt. Joachim Kilemile amesema ni uzee, kisukari pamoja na shinikizo la juu la damu.

Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila katika jitihada zake za kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi inatarajia kufanya huduma mkoba (outreach) katika Viwanja vya Nane Nane mkoani Dodoma kuanzia Agost 1 hadi 8, 2025.

Chapisha Maoni

0 Maoni